
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kile kilichoelezwa kuwa ni mafanikio katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ushawishi wake katika jukwaa la kimataifa na kuimarisha imani ya taasisi za kimataifa kwa Tanzania.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, ambaye amesema uamuzi wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika kufanya mkutano wao nchini Tanzania ni uthibitisho wa kuongezeka kwa hadhi na kuaminika kwa nchi chini ya uongozi wa Rais Samia.
Mbeto alisema Serikali ya Rais Samia imefanikiwa kufikia malengo ya maendeleo kupitia usimamizi thabiti wa sera na utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayovutia uwekezaji wa ndani na nje.
Alieleza kuwa Taasisi ya Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika vina mchango mkubwa katika kuharakisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi pamoja na kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali za kifedha.

Kwa mujibu wa Mbeto, mikakati ya Serikali ya kushirikisha mitaji ya sekta binafsi katika uwekezaji imeifanya Tanzania kuwa kivutio cha uwekezaji, hususan katika sekta za nishati, usafirishaji na gesi asilia, hatua ambayo imeendelea kuimarisha maendeleo ya uchumi wa taifa.
“Juhudi za Serikali katika kuharakisha ujenzi wa miundombinu na kukamilisha miradi ya kimkakati kwa viwango vya kimataifa zinaendelea kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri miongoni mwa mataifa ya Afrika,” alisema Mbeto.
Aidha, alisema mafanikio hayo yanathibitisha kuwa Tanzania ni eneo salama kwa uwekezaji na yanatoa ujumbe chanya kwa jumuiya ya kimataifa kuhusu fursa zilizopo nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Mbeto pia aliwataka wanaobeza mafanikio ya Serikali kutambua kuwa taasisi za kimataifa zinaendelea kuonyesha imani kwa Tanzania kupitia ushirikiano na uwekezaji unaoendelea kushuhudiwa.
Kauli hiyo imetolewa wakati viongozi mbalimbali kutoka nchi za Afrika wakihudhuria Mkutano wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mgeni rasmi na mwenyeji wa mkutano huo.