
Shirika la mchezo wa mapigano la UFC limepata hasara ya takribani dola milioni 30, sawa na zaidi ya Sh bilioni 78 za Tanzania, kutokana na gharama za kuandaa tukio maalumu la Freedom 250 lililofanyika katika Ikulu ya Marekani (White House) mwezi Juni 2026.
Kwa mujibu wa kampuni mama ya UFC, TKO Group Holdings, tukio hilo lililofanyika Juni 14, 2026, siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Rais wa Marekani Donald Trump kutimiza miaka 80, liligharimu fedha nyingi zaidi kuliko matukio ya kawaida ya UFC.
Afisa Mkuu wa Fedha wa TKO Group Holdings, Andrew Schleimer, aliwaeleza wawekezaji kuwa gharama kubwa za uzalishaji wa tukio hilo ziliathiri mapato ya kampuni.

Tukio hilo lilifanyika kwenye eneo la South Lawn la White House na lilihudhuriwa na takribani watu 4,300, wakiwemo viongozi, wafanyabiashara maarufu na mastaa mbalimbali.
Miongoni mwa waliohudhuria walikuwa Makamu wa Rais JD Vance, mwanzilishi wa Facebook na Mkurugenzi Mkuu wa Meta, Mark Zuckerberg mmiliki wa New York, Knicks James Dolan, mmiliki wa New England Patriots, Robert Kraft pamoja na mchekeshaji Shane Gillis.

Licha ya hasara hiyo, UFC ilitarajia kupata changamoto za kifedha kutokana na ukubwa wa tukio hilo, ambalo lilikuwa la kipekee kwa kufanyika katika eneo la White House na kurushwa moja kwa moja kupitia Paramount+.
Tiketi za kawaida hazikuuzwa kwa umma, ingawa baadhi ya vifurushi maalumu vya wageni wenye uwezo mkubwa kifedha viliripotiwa kuwepo kwa ajili ya kupata nafasi za kipekee.