×

Rais Samia na Museveni Washuhudia Makubaliano ya Mradi wa Nishati Tanga

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, leo wameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) ya kuendeleza ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta na Kitovu cha Nishati cha Kikanda mjini Tanga, mradi unaotarajiwa kuimarisha sekta ya nishati na uchumi wa Afrika Mashariki.

Makubaliano hayo yamesainiwa kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na kampuni ya VTTO Bahrain, yakifungua njia ya maandalizi ya kitaalamu na uwekezaji wa ujenzi wa miundombinu hiyo muhimu.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Waziri wa Nishati, Deogratias Ndejembi, alisema hatua hiyo ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano wa Tanzania na Uganda katika sekta ya nishati.

Alieleza kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta, miundombinu ya kuhifadhi bidhaa za petroli, huduma za usafirishaji pamoja na bomba la kusafirisha bidhaa za mafuta litakaloweza kufanya kazi kwa pande zote mbili kati ya Tanzania na Uganda.

Kwa mujibu wa Ndejembi, utekelezaji wa mradi huo unalenga kuifanya Tanga kuwa kitovu kikuu cha usambazaji wa bidhaa za mafuta kwa nchi za Afrika Mashariki na maeneo mengine ya bara la Afrika.

“Utiaji saini wa leo siyo tu makubaliano, bali ni msingi mwingine wa mageuzi ya kiuchumi katika Afrika Mashariki,” alisema.

Alibainisha kuwa mradi huo unaendeleza ushirikiano ulioanzishwa kupitia Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), wenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni sita, unaosafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Tofauti na EACOP inayolenga usafirishaji wa mafuta ghafi, alisema Kitovu cha Nishati cha Tanga kitaongeza thamani ya rasilimali hiyo kupitia usafishaji wa mafuta, uhifadhi, usafirishaji na biashara ya bidhaa za petroli.

Aidha, alisema mradi huo unatarajiwa kuvutia uwekezaji unaozidi dola za Marekani bilioni 20, kuunda maelfu ya ajira, kuchochea ukuaji wa viwanda na kuimarisha usalama wa nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dk. Ruth Nankabirwa Ssentamu, alisema makubaliano hayo yanaonesha dhamira ya Tanzania na Uganda ya kuongeza thamani ya rasilimali za mafuta badala ya kuuza malighafi pekee.

Alisisitiza kuwa kiwanda cha kusafisha mafuta kinachotarajiwa kujengwa Kabaale nchini Uganda na Kitovu cha Nishati cha Tanga havitakuwa washindani, bali vitasaidiana kuongeza uwezo wa usafishaji wa mafuta na kuimarisha upatikanaji wa nishati katika Afrika Mashariki.

Mbali na mradi huo, Tanzania na Uganda zinaendelea kutekeleza miradi mingine ya pamoja ikiwemo bomba la kusafirisha bidhaa za mafuta, bomba la gesi asilia kati ya nchi hizo mbili na mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 400.

Utiaji saini wa makubaliano hayo unaongeza hatua mpya katika ushirikiano wa muda mrefu wa Tanzania na Uganda kwenye sekta ya nishati, ulioanza kuimarika kupitia utekelezaji wa mradi wa EACOP mwaka 2017.

Leave a Comment