
Nyota wa TikTok, Sydney Towle, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 26 baada ya kuishi kwa miaka mitatu akipambana na saratani ya mirija ya nyongo (cholangiocarcinoma).
Taarifa za kifo chake zilitolewa kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii leo Alhamisi, Agosti 6, 2026, siku moja baada ya kufariki kwake.
Familia yake ilisema katika ujumbe huo kuwa walijivunia namna alivyopambana na ugonjwa huo, wakimtaja Sydney kama mwanga wa furaha usio na mwisho na mtu aliyekuwa binti, dada na rafiki wa wengi.
Sydney aligunduliwa na saratani ya mirija ya nyongo akiwa na umri wa miaka 23, aina ambayo mara nyingi huwapata watu wenye umri mkubwa zaidi ya miaka 50.
Baada ya utambuzi huo, alianza kushiriki safari yake ya matibabu kupitia TikTok na Instagram, ambako alijenga jumuiya zaidi ya wafuasi milioni moja.

Katika kipindi cha mapambano yake, Sydney alipitia upasuaji kadhaa, matibabu ya kemikali (chemotherapy) na kushiriki katika tafiti mbalimbali za tiba mpya. Alisema awali kuwa kushiriki maisha yake mtandaoni kulimpa “kusudi” na kuwasaidia wengine waliokuwa wakipitia changamoto kama zake.
Mwaka 2026, hali yake ilizidi kuwa mbaya baada ya madaktari kubaini kuwa saratani ilikuwa imesambaa katika sehemu ya ndani ya tumbo (peritoneum). Baadaye alieleza kuwa daktari wake alipendekeza aanze huduma za mwisho wa maisha (hospice), jambo lililomshtua yeye na familia yake.
Hata hivyo, Sydney hakukata tamaa na aliamua kutafuta mtaalamu mwingine huku akiendelea na juhudi za matibabu kupitia majaribio ya tiba maalum.

Miezi michache kabla ya kifo chake, Sydney pia alishiriki katika maonesho ya mavazi ya kuogelea ya Chemo Club x Post Swim wakati wa Miami Swim Week, akilenga kuhamasisha wanawake wenye makovu au mabadiliko ya mwili kutokana na matibabu ya saratani kujikubali.
Kabla ya kifo chake, Sydney aliendelea kushiriki ujumbe wa matumaini na kuonyesha maisha yake ya kila siku akiwa na familia na marafiki.
Kaka yake, Austin Towle, alitangaza awali kuwa dada yake alikuwa amepelekwa kwenye huduma ya uangalizi wa mwisho akiwa amezungukwa na wapendwa wake.
Sydney Towle ameacha historia ya kuwa mmoja wa watengeneza maudhui waliotumia jukwaa la mitandao ya kijamii kuelimisha kuhusu saratani adimu na kutoa matumaini kwa wagonjwa wengine duniani.