
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amezindua Tume ya Uchunguzi wa Wahusika wa Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria katika matukio ya ghasia yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Rais Samia amesema tume hiyo imepewa muda wa miezi mitano kukamilisha uchunguzi wake na kuwasilisha mapendekezo yatakayosaidia kufahamu chanzo cha matukio hayo pamoja na wahusika wake.

Akizindua tume hiyo, Rais Samia amewataka Watanzania kutoa ushirikiano kwa wajumbe wa tume ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
“Niwasihi sana Watanzania wote kutoa ushirikiano unaohitajika na tume katika kutekeleza majukumu yao. Tuisaidie tume hii iweze kufanya kazi yake na tusiisumbue,” amesema Rais Samia.
Tume hiyo inalenga kuchunguza matukio ya ghasia na ukiukwaji wa sheria yaliyotokea katika kipindi cha uchaguzi, kubaini wahusika na kutoa mapendekezo kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa.

