×

Mtoto wa Miaka 12 Aokoka Kifo Baada ya Kuburutwa Chini ya Lori Kubwa Brazil

Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 12 nchini Brazil amenusurika katika ajali ya kutisha baada ya kuvutwa na lori kubwa na kuangukia chini ya magurudumu yake, lakini kwa bahati ya ajabu aliweza kusimama na kutembea baada ya tukio hilo.

Tukio hilo la kushtua lilitokea katika mji wa Firminópolis, jimbo la Goiás nchini Brazil, wakati mtoto huyo alipokuwa akitoka shule akielekea nyumbani akiwa akisukuma baiskeli yake.

Kwa mujibu wa taarifa, koti la mtoto huyo lilinaswa na lori aina ya Volvo FH 540 lililokuwa likipita eneo hilo wakati likielekea kuingia kwenye barabara kuu ya GO-060.

Nguvu ya lori hilo lilimvuta mtoto huyo na kumuangusha chini, huku baiskeli yake ikirushwa pembeni. Kamera za ulinzi zilinasa tukio hilo la kutisha, zikionyesha mtoto huyo akipita chini ya sehemu ya lori hilo lenye magurudumu makubwa.

Katika hali iliyowashangaza wengi, mtoto huyo hakupata majeraha makubwa yaliyotarajiwa kutokana na ajali hiyo. Baada ya lori kupita, alionekana akiinuka na kutembea kutoka eneo la tukio.

Watu waliokuwa karibu, wakiwemo wafanyakazi wa duka la dawa lililopo jirani, walikimbia kwenda kumsaidia na kumpatia huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa hospitalini.

Madaktari katika Hospitali ya Santa Gemma walieleza kuwa mtoto huyo alipata kuvunjika mkono wa kushoto pamoja na michubuko kwenye kiwiko. Baadaye alihamishiwa katika Hospitali ya Dharura ya Jimbo la Goiás, Hospitali ya Dr Valdemiro Cruz (Hugol), kwa matibabu zaidi.

Dereva wa lori hilo hakusimama mara moja baada ya tukio hilo, lakini baadaye aliwasiliana na polisi baada ya kupata video ya ajali hiyo kutoka kwa rafiki yake.

Dereva huyo alisema hakuwa amegundua kuwa alikuwa amegonga mtoto huyo, akidai kuwa mtoto huyo alikuwa kwenye eneo ambalo halikuonekana kupitia vioo vya lori.

Aliwaeleza polisi kuwa yuko tayari kushirikiana na familia ya mtoto huyo na kusaidia katika gharama za matibabu.

Vyombo vya usalama nchini Brazil vinaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini mazingira kamili ya ajali hiyo.

Leave a Comment