
Barcelona imewasilisha ofa ya kwanza ya pauni milioni 38.5 (TSh bilioni 137) kwa Manchester City kwa ajili ya kiungo wa kati wa Hispania, Rodri, lakini ofa hiyo imekataliwa.
Manchester City iko tayari kumuuza nyota huyo mwenye umri wa miaka 30, ambaye mkataba wake unakaribia kumalizika, lakini klabu hiyo inataka zaidi ya pauni milioni 60 (TSh bilioni 213.5) kabla ya kumruhusu kuondoka Etihad.
Rodri hajatia saini mkataba mpya na City, jambo lililoongeza uvumi kuhusu mustakabali wake katika dirisha hili la usajili.
Awali, Real Madrid ilionekana kuwa klabu yenye nafasi kubwa zaidi ya kumsajili, lakini sasa Barcelona imeongoza mbio hizo baada ya kupata ridhaa ya mchezaji kuanza mazungumzo na Manchester City.
BBC Sport inaripoti kuwa Barcelona iliwasilisha ofa yake ya kwanza siku ya Ijumaa, huku mazungumzo kati ya klabu hiyo na wawakilishi wa Rodri yakiendelea.
Wakati huo huo, mazungumzo ya Rodri na Real Madrid yamefikia mwisho.

Real Madrid ilitoa ofa iliyokuwa “isiyoweza kukataliwa”
Kwa mujibu wa kituo cha redio cha Hispania, Cadena SER, wakizungumza na wakala wa Rodri, Pablo Barquero, Real Madrid ilimpa mchezaji huyo ofa kubwa muda mfupi baada ya Hispania kushinda Kombe la Dunia.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Real Madrid ilikuwa imedhamiria sana kumpata Rodri, huku viongozi wakuu wa klabu hiyo wakishiriki katika kuhakikisha dili hilo linafanikiwa.
Hata hivyo, licha ya mazungumzo kuwa mazuri kwa wiki kadhaa, Rodri amefanya uamuzi binafsi wa kukubali ofa nyingine.
Real Madrid ilifahamishwa kuhusu uamuzi huo siku ya Ijumaa na ikaamua kusitisha mchakato huo ili kuepusha kuendelea kwa sintofahamu kuhusu mustakabali wa mchezaji huyo.
Rodri bado ni tegemeo la City
Rodri amekuwa na changamoto za majeraha katika misimu ya hivi karibuni. Alikosa sehemu kubwa ya msimu wa 2024/25 kutokana na jeraha kubwa la goti, huku msimu uliopita pia ukivurugwa na tatizo la misuli ya paja.
Licha ya changamoto hizo, alirejea katika kiwango chake bora kwenye Kombe la Dunia, ambako aliiongoza Hispania kutwaa ubingwa wa pili na pia akachaguliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano.
Kwa sasa Rodri yuko nje ya uwanja baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo mwezi uliopita. Anatarajiwa kurejea Manchester mwanzoni mwa wiki ijayo kuungana tena na wachezaji wenzake wa City.
Manchester City sasa inataka kupata uamuzi kuhusu mustakabali wake haraka ili iweze kupata mbadala wake kabla dirisha la usajili halijafungwa.
City pia inaendelea na mazungumzo ya kumsajili kiungo wa miaka 18 wa Lille, Ayyoub Bouaddi, lakini dau la pauni milioni 86 linalotakiwa na klabu hiyo ya Ufaransa limekuwa kikwazo.