
DAR ES SALAAM: Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amelalamikia ucheleweshwaji wa mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili, akidai kuwa upande wa Jamhuri umechangia kuchelewa kwa kesi hiyo kwa kufungua maombi ya marejeo katika Mahakama ya Rufani.
Lissu ametoa kauli hiyo leo, Agosti 10, 2026, mara baada ya kuanza kwa kesi hiyo katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, mbele ya Jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.
Akizungumza mahakamani, Lissu amesema kesi hiyo imepoteza muda wa siku 166 tangu ilipopelekwa Mahakama ya Rufani, akidai kuwa hatua hiyo ilichelewesha kuendelea kwa mwenendo wa shauri.

“Leo majaji ni siku ya 166 tangu tarehe 24 Februari 2026 wamekwenda Mahakama ya Rufani. Nimewashinda, lakini tumerudi baada ya kupotezeana siku 166. Tuendelee, lakini itakapofika siku itabidi tuzungumze hii kesi ya bure na huu ucheleweshaji wa bure uliofanywa na mawakili na anayewatuma. Someone has to pay for this,” amesema Lissu.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri umepinga madai hayo.
*Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, amesema si sahihi kusema kuwa upande wa Jamhuri ulikuwa na nia ya kuchelewesha kesi, akieleza kuwa hatua ya kuomba marejeo katika Mahakama ya Rufani ilikuwa ni haki ya kisheria ya upande huo.

Kwa mujibu wa Katuga, Jamhuri iliwasilisha maombi hayo baada ya kuona kuwa kulikuwa na maeneo ambayo iliamini hayakuamuliwa kwa usahihi na Mahakama.
“Haikuwa nia ya upande wa Jamhuri kuchelewesha kesi. Kuhusu kushinda na kushindwa, kushindwa kwa wakili mwenye weledi ni jambo la kawaida,” amesema Katuga.
Baada ya kusikiliza maelezo ya pande hizo, Jaji Dunstan Ndunguru alielekeza mwenendo wa kesi kuendelea.
Kwa sasa, shahidi wa upande wa Jamhuri, ACP Amini Mahamba, anaendelea kutoa ushahidi wake mbele ya Mahakama.
Kesi hiyo inaendelea katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.