
Pazia la NBC Premier League msimu wa 2026/27 linatarajiwa kufunguliwa rasmi Agosti 14, huku timu mbalimbali zikianza kampeni ya kusaka pointi tatu katika ratiba yenye michezo kadhaa ya kuvutia na yenye ushindani mkubwa.
Simba ni miongoni mwa timu zinazokabiliwa na ratiba ya moto katika michezo yake ya mwanzo, baada ya kumaliza msimu uliopita katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 73, nyuma ya mabingwa Yanga SC waliomaliza na pointi 75.
Mnyama atafungua kampeni yake Agosti 16 kwa mchezo dhidi ya Kagera Sugar, timu iliyopanda daraja kutoka Championship, katika Uwanja wa Kaitaba.
Baada ya hapo, Simba itakuwa ugenini tena Agosti 19 dhidi ya Pamba Jiji FC katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, kabla ya Agosti 22 kukutana na Singida Black Stars katika Uwanja wa Airtel.
Simba na Singida tayari zimekutana kwenye Kagame Cup, ambapo Wekundu wa Msimbazi waliibuka na ushindi wa mabao 2-1, lakini safari hii watakutana katika mchezo wa ligi.

Mchezo wa kwanza wa Simba nyumbani utakuwa Agosti 27 dhidi ya Coastal Union katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kabla ya kumaliza michezo yake mitano ya mwanzo Agosti 31 kwa kuikabili Geita Gold katika uwanja huo huo.
Simba, inayofundishwa na Kocha Mkuu Steve Barker, inalenga kuanza msimu kwa nguvu katika mbio za kuwania ubingwa.
Kwa upande wa TRA United, timu hiyo inaanza msimu ikiwa na ratiba yenye changamoto, ikitarajiwa kucheza mechi tatu ugenini na mbili nyumbani katika michezo yake mitano ya mwanzo.
TRA United itaanza kampeni Agosti 16 dhidi ya JKT Tanzania katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, kuanzia saa 2:30 usiku.
Agosti 20 itakutana na Azam FC katika Azam Complex, kabla ya kusafiri kwenda Tanga Agosti 24 kucheza dhidi ya Coastal Union katika Uwanja wa CCM Mkwakwani.
Mchezo mwingine utakuwa dhidi ya Dodoma Jiji Agosti 29 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, kabla ya kukutana na Mbeya City Septemba 4 katika uwanja huo huo.

TRA United itafunga michezo yake mitano ya mwanzo kwa kukutana na Pamba Jiji Septemba 13 katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, kuanzia saa 10:00 jioni.
Geita Gold yenyewe inatarajiwa kuanza msimu kwa kucheza michezo miwili ya mwanzo ugenini kabla ya kurejea nyumbani katika Uwanja wa Bukombe, Geita.
Mchezo wa kwanza utakuwa dhidi ya Mbeya City Agosti 14 katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, kabla ya Agosti 18 kukutana na Namungo katika Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa.
Agosti 22, Geita Gold itacheza mchezo wake wa kwanza nyumbani dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Bukombe, ambao pia utakuwa miongoni mwa michezo ya mwanzo kwa timu hiyo kutumia uwanja huo mpya uliofunguliwa mwaka huu.
Agosti 28, Geita Gold itakuwa na mtihani mwingine mzito itakapokutana na Azam FC katika Uwanja wa Bukombe, kabla ya Agosti 31 kusafiri kwenda Dar es Salaam kukabiliana na Simba SC katika Uwanja wa Uhuru.
Coastal Union ya Tanga, maarufu kama Wagosi wa Kaya, nayo iko tayari kwa msimu mpya ikiwa na michezo mitano ya mwanzo inayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Coastal Union itafungua kampeni Agosti 15 kwa kuikabili Mashujaa FC katika Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga, kabla ya Agosti 20 kusafiri kwenda Dar es Salaam kucheza dhidi ya mabingwa watetezi Yanga SC katika Uwanja wa Uhuru.
Agosti 24 itakuwa nyumbani kuikaribisha TRA United katika Uwanja wa CCM Mkwakwani, huku Agosti 27 ikirejea Dar es Salaam kukabiliana na Simba SC katika Uwanja wa Uhuru.
Mchezo wa tano utakuwa Septemba 6 dhidi ya Polisi Tanzania katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Pamba Jiji FC nayo imepewa ratiba ngumu katika michezo yake mitano ya mwanzo, huku timu hiyo ya Mwanza inayofundishwa na Kocha Mkuu Francis Baraza ikikutana na baadhi ya timu zinazotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa msimu huu.
Pamba Jiji itaanza Agosti 14 dhidi ya Dodoma Jiji katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, kabla ya Agosti 19 kukutana na Simba SC katika uwanja huo huo.
Agosti 23, Pamba Jiji itacheza mchezo wake wa kwanza ugenini dhidi ya Azam FC katika Azam Complex, Dar es Salaam.
Baada ya hapo, Agosti 28 itakutana na mabingwa watetezi Yanga SC katika Uwanja wa Uhuru, kabla ya Septemba 5 kucheza dhidi ya JKT Tanzania katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Mashujaa FC, inayotumia Uwanja wa Lake Tanganyika kwa mechi zake za nyumbani, inaanza msimu ikiwa na ratiba yenye changamoto katika michezo yake mitano ya mwanzo.
Mchezo wa kwanza utakuwa Agosti 15 dhidi ya Coastal Union katika Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga, kuanzia saa 12:30 jioni.
Agosti 18, Mashujaa itasafiri kwenda Arusha kucheza dhidi ya Fountain Gate katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, kuanzia saa 10:00 jioni.
Agosti 23 itakutana na Mbeya City katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, kabla ya kurejea nyumbani Agosti 27 kuikaribisha Kagera Sugar katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Mchezo wa tano utakuwa Septemba 4 dhidi ya Dodoma Jiji katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Dodoma Jiji FC itafungua kampeni yake Agosti 14 kwa mchezo dhidi ya Pamba Jiji katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Timu hiyo inayotumia Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kama uwanja wake wa nyumbani tayari ipo kambini Arusha ikiendelea na maandalizi ya msimu mpya.
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Moses Mpunga, amesema maandalizi yanaendelea vizuri kuelekea msimu mpya.
Baada ya mchezo dhidi ya Pamba Jiji, Dodoma Jiji itacheza dhidi ya Mbeya City Agosti 19 katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, kabla ya kurejea nyumbani Agosti 25 kuikaribisha Polisi Tanzania katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Agosti 29, Dodoma Jiji itakuwa ugenini dhidi ya TRA United katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, kabla ya Septemba 4 kukutana na Mashujaa FC.
JKT Tanzania nayo itaanza msimu Agosti 16 kwa kuikaribisha TRA United katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Agosti 20, JKT itacheza mchezo wake wa kwanza ugenini dhidi ya Polisi Tanzania katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha. Polisi Tanzania imefanikiwa kurejea Ligi Kuu baada ya kushiriki Championship.
Mchezo wa tatu wa JKT Tanzania utakuwa Agosti 24 dhidi ya mabingwa watetezi Yanga SC, ambao wanaingia kwenye msimu mpya wakiwa wamefanya usajili wa wachezaji mbalimbali wenye majina makubwa, akiwemo mshambuliaji Peter Shalulile aliyewahi kuitumikia Mamelodi Sundowns.
Agosti 29, JKT Tanzania itakuwa nyumbani kuikaribisha Namungo FC, kabla ya Septemba 5 kumaliza michezo yake mitano ya mwanzo kwa kuikabili Pamba Jiji katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Kwa ujumla, ratiba ya mwanzo ya NBC Premier League 2026/27 inaonesha kuwa timu nyingi zimeanza msimu zikiwa na mitihani mikubwa, huku Simba, Pamba Jiji, Coastal Union, Geita Gold, TRA United, Mashujaa, Dodoma Jiji na JKT Tanzania zikilazimika kutumia vyema michezo hiyo ya mwanzo katika msako wa pointi muhimu.
Waandishi: Avia Kyaruzi, Lailath Burhan, Kayanda Idd, Nasra Kassim, Tereza Muga na Witness Wilbert.