×

Sakata la Bando: Shigongo Apeleka Malalamiko TCRA, Atoa Siku 90, Mahakama Yatajwa

DAR ES SALAAM: Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo, amesema amewasilisha rasmi malalamiko katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhusu suala la vifurushi vya intaneti, maarufu kama bando, kupotea.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Shigongo amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kubaini kuwa hawezi kufungua kesi moja kwa moja mahakamani bila kwanza kuwasilisha malalamiko katika mamlaka husika.

Shigongo amesema kupitia mawakili wake kutoka SLA Legal Advisory, amewasilisha barua ya malalamiko TCRA kwa niaba ya wananchi.

Amesema kwa mujibu wa utaratibu wa kisheria, endapo malalamiko hayo hayatapatiwa ufumbuzi katika hatua ya TCRA, ndipo hatua ya kwenda mahakamani itafuata.

“Wiki iliyopita kupitia kwa mawakili wangu SLA Legal Advisory, niliwakilisha kwa niaba yenu barua ya malalamiko Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA),” amesema Shigongo.

Mbunge huyo amesema ametoa muda wa siku 90 kwa mchakato huo, baada ya hapo anatarajia kuchukua hatua za kisheria mahakamani iwapo suala hilo halitapatiwa ufumbuzi.

Hatua hiyo inakuja wakati malalamiko kuhusu matumizi na upotevu wa vifurushi vya intaneti yakiendelea kujadiliwa na watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini.

Shigongo amewashukuru wananchi kwa ushirikiano wao na kusema anaendelea kufuatilia suala hilo kwa niaba yao.

Leave a Comment