
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametembelea banda la Kampuni ya Mawasiliano Yas wakati wa Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi yaliyofanyika Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Rais Samia alitembelea banda hilo Agosti 12, 2026, ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na kufahamu shughuli mbalimbali zinazofanywa na kampuni hiyo katika kuchangia maendeleo ya sekta ya mawasiliano na uchumi wa kidijitali.
Yas ni miongoni mwa wadau muhimu katika kukuza Uchumi wa Buluu na sekta ya utalii Zanzibar, kupitia uwekezaji wake katika miundombinu ya mawasiliano pamoja na huduma mbalimbali za kidijitali.
Uwekezaji huo unalenga kuimarisha muunganisho wa mawasiliano na kuwezesha matumizi ya teknolojia katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo utalii.
Sekta ya utalii ikiwa miongoni mwa maeneo muhimu yanayochangia uchumi wa Zanzibar, uwepo wa huduma bora za mawasiliano unaendelea kuwa sehemu muhimu katika kuwahudumia watalii, wafanyabiashara na wananchi.
Ziara ya Rais Samia katika banda la Yas imefanyika sambamba na shughuli za Tamasha la Kizimkazi, ambalo limekuwa jukwaa la kuonesha fursa, bidhaa, huduma na shughuli mbalimbali zinazochangia maendeleo ya Zanzibar.