×

Steve Barker Akiri Makosa Baada ya Simba Kupoteza kwa Yanga

Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amekiri kuwa kuna mambo yaliyohitaji kufanyiwa kazi baada ya kikosi chake kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga SC katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa Jumatano, Agosti 12, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Simba ilipoteza mchezo huo baada ya Yanga kupata bao pekee kupitia Albert Kangwanda dakika ya 31, akifunga kwa kichwa kufuatia krosi iliyopigwa na beki wa kushoto, Chadrack Boka.

Bao hilo lilitosha kuipa Yanga ushindi na kuiwezesha kutetea taji la Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo, huku Simba ikishindwa kurejesha taji hilo ambalo ililitwaa mara ya mwisho mwaka 2023.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Barker amekiri kuwa matokeo hayo yameonyesha maeneo ambayo Simba inapaswa kuyafanyia kazi kabla ya kuanza rasmi kwa msimu wa NBC Premier League 2026/27.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini sasa anatarajiwa kutumia mchezo huo kama kipimo cha kutathmini kikosi chake, hasa katika maeneo ambayo yalionekana kuwa na mapungufu wakati wa mchezo huo wa kwanza wa ushindani msimu huu.

Kwa upande mwingine, ushindi huo umeendelea kuipa Yanga morali kubwa kuelekea msimu mpya, huku Kocha Manqoba Mngqithi akiibuka mshindi katika pambano la kwanza dhidi ya Barker.

Mchezo huo pia ulikuwa wa kihistoria kutokana na kuwakutanisha kwa mara ya kwanza makocha hao wawili kutoka Afrika Kusini wakiwa kwenye benchi za klabu mbili kubwa za Tanzania.

Kwa Yanga, ushindi huo umeendeleza utawala wake katika Ngao ya Jamii, wakati kwa Simba na Barker, kipigo hicho kimekuwa ishara ya mapema kwamba bado kuna kazi ya kufanya kabla ya kuanza mbio za ubingwa wa NBC Premier League.

Simba itahitaji kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza dhidi ya Yanga na kuhakikisha kikosi kinakuwa tayari kwa ratiba ya msimu mpya, ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Stori na Na Anifa mwegelo | GPL

Leave a Comment