
ORYX Gas Zanzibar imeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, ambapo kampuni hiyo imetoa mitungi ya gesi kwa wananchi wakati wa Tamasha la Kizimkazi lililofanyika Zanzibar.
Akizungumza katika kongamano la nishati safi lililofanyika sambamba na Tamasha la Kizimkazi, Meneja Mkuu wa ORYX Gas Zanzibar, Shuwekha Khamis, alisema kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kuhamasisha matumizi ya gesi ya LPG katika taasisi na maeneo mbalimbali ya Zanzibar.
Alisema ORYX Gas imefanikiwa kusaidia kubadilisha matumizi ya nishati katika taasisi mbalimbali, ikiwemo shule 25, pamoja na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), ambako imewezesha mabadiliko katika kambi sita zilizopo Unguja na Pemba.
“Tumekuwa tukizisaidia taasisi katika mabadiliko na hapa Zanzibar ORYX tumeshapiga hatua kuzibadilisha baadhi ya taasisi zikiwemo shule 25. Pia JKU kuna kambi sita Unguja na Pemba,” alisema.
Shuwekha aliongeza kuwa kampuni hiyo, kwa kushirikiana na Mwanamke Initiative Foundation, imewezesha mabadiliko ya matumizi ya nishati katika Gereza la Kiinua Mguu, vituo viwili vya polisi, vituo 12 vya afya pamoja na baadhi ya ofisi za Serikali na taasisi nyingine.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, Zanzibar imepiga hatua katika matumizi ya LPG, ambapo matumizi ya nishati safi ya kupikia yameongezeka kutoka takribani asilimia sita mwaka 2020 hadi zaidi ya asilimia 30 mwaka 2025.
Alisema ongezeko hilo limetokana na ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wengine katika kuhamasisha wananchi kuachana na nishati zinazochafua mazingira na kutumia nishati safi.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, ORYX Gas Zanzibar imetoa mitungi ya gesi kwa wananchi waliotembelea Tamasha la Kizimkazi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhamasisha matumizi ya LPG.
Kampuni hiyo pia imeeleza kuwa inaandaa mpango wa kusaidia hoteli na viwanda Zanzibar kuhamia kwenye matumizi ya majenereta yanayotumia gesi ya LPG, hatua inayolenga kuongeza matumizi ya nishati safi katika sekta za uzalishaji na biashara.
Tamasha la Kizimkazi lilianza Agosti 12 na kuhitimishwa Agosti 14, 2026, likiwa na shughuli mbalimbali ikiwemo kongamano lililojadili umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Juhudi hizo zinaendana na mkakati wa Serikali wa kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni pamoja na lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar