
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema ataitangaza hivi karibuni mlango wa bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani baada ya kile alichodai kuwa ni ushindi wa nchi yake dhidi ya Iran, kauli ambayo huenda ikaongeza zaidi mvutano kati ya Washington na Tehran.
Trump alitoa kauli hiyo Ijumaa, Agosti 14, 2026, wakati akihutubia mkutano wa kisiasa katika Chuo cha Polisi jijini Garden City, New York, akisema Marekani iko katika harakati za kuishinda Iran.
“Baada ya kumaliza kuishinda Iran, ambayo inashindwa vibaya sana, hivi karibuni nitatangaza Strait ya Hormuz kuwa eneo la Marekani,” Trump alisema huku akicheka, na kuongeza: “Ni kweli.”
Hormuz ni njia muhimu ya baharini inayounganisha Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman na ni miongoni mwa njia muhimu zaidi duniani kwa usafirishaji wa mafuta na gesi.

Mvutano kuhusu njia hiyo umeongezeka tangu kuanza kwa vita kati ya Marekani, Israel na Iran. Iran imedhibiti kwa kiasi kikubwa usafirishaji katika eneo hilo, huku Marekani ikiendesha kizuizi cha majini dhidi ya bandari za Iran.
Trump pia amesisitiza kuwa Marekani ina udhibiti wa kizuizi hicho, akisema hakuna meli inayoweza kupita isipokuwa kwa ridhaa ya Marekani.
Kauli hiyo imekuja wakati usafirishaji kupitia Strait ya Hormuz ukiwa umepungua kwa kiwango kikubwa, hali ambayo imeathiri soko la nishati duniani na kuongeza shinikizo la bei ya mafuta. Reuters imeripoti kuwa ni meli chache sana zilizopita katika njia hiyo siku ya Ijumaa ikilinganishwa na kiwango cha kawaida cha takribani meli 130 kwa siku kabla ya vita.
Trump pia amewataka Wamarekani kukubali kuongezeka kwa bei ya petroli, akisema gharama hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha Iran haipati silaha za nyuklia. Alisema hatatoa msamaha kwa hatua ya kuishambulia Iran, akisisitiza kuwa Marekani inafanya “huduma kubwa kwa dunia.”
Hata hivyo, Iran imepinga madai ya Marekani kuhusu udhibiti wa Strait ya Hormuz, huku viongozi wake wakisisitiza kuwa mamlaka juu ya njia hiyo hayawezi kuamuliwa na Washington.
Kauli ya Trump kuhusu kuitangaza Strait ya Hormuz kuwa eneo la Marekani imeongeza mzozo mwingine wa kisiasa na kisheria katika mgogoro huo, huku ikiwa haijaelezwa wazi namna hatua hiyo ingetekelezwa au kutambuliwa chini ya sheria za kimataifa.