Huduma ya Airtel Money School Pay imeendelea kurahisisha ulipaji na ukusanyaji wa ada za wanafunzi nchini, huku zaidi ya shule 800 kutoka mikoa 16 tayari zikiwa zimejiunga na kutumia mfumo huo wa kidijitali.
Mfumo huo unalenga kuwawezesha wazazi kulipa ada kwa urahisi, huku shule zikipata njia salama na yenye ufanisi ya kusimamia malipo na taarifa za kifedha.
Akizungumza wakati wa ziara katika Salaam Pre and Primary School, iliyopo Chamazi, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Afisa Huduma wa Airtel Money School Pay, Roda William Mganga, alisema huduma hiyo ilianzishwa mwaka 2024 kwa lengo la kutoa njia rahisi, salama na yenye ufanisi katika ulipaji wa ada na usimamizi wa taarifa za malipo.
Mganga alisema tangu kuanzishwa kwake, School Pay imefikia zaidi ya shule 800 katika mikoa 16 nchini, huku Airtel ikiwa na lengo la kuunganisha shule 1,000 kila mwaka.
Mikoa ambayo tayari imefikiwa na huduma hiyo ni pamoja na Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Mbeya, Arusha, Mwanza na Mtwara.
Alisema baadhi ya shule zinazotumia mfumo huo ni St. Anne Maria Academy, Fountain Gate Schools, St. Anthony’s Secondary School, Salaam Pre and Primary School, Living Minds Pre and Primary School, Memon Pre and Primary School na Mbwawa Lutheran Secondary School.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Salaam Pre and Primary School, Kalunji Mkasa Idris, alisema shule hiyo imekuwa ikitumia School Pay tangu Septemba mwaka jana na kwamba mfumo huo umeleta mabadiliko katika ukusanyaji na usimamizi wa ada.
Alisema awali shule hiyo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto za kupokea fedha taslimu, hali iliyoongeza hatari ya fedha kupotea na kufanya ufuatiliaji wa malipo kuwa mgumu.
“School Pay imetusaidia sana katika ukusanyaji wa ada. Sasa fedha zinazoingizwa kupitia mfumo zinaonekana na kuingia benki, hivyo tunapata kumbukumbu sahihi na tunakuwa na uwezo wa kuzitumia kwa mahitaji ya shule,” alisema Idris.
Aidha, alisema mfumo huo umewarahisishia wazazi kwa kuwa hawalazimiki tena kwenda benki na kusimama kwenye foleni kwa ajili ya kulipa ada.
Kwa kutumia simu zao, wazazi wanaweza kufanya malipo wakati wowote, ikiwemo nyakati za usiku, huku taarifa za malipo zikionekana kwenye mfumo wa shule ndani ya muda mfupi na kurahisisha utoaji wa risiti pamoja na ufuatiliaji wa malipo.
Mhasibu wa Salaam Pre and Primary School, Fatma Yusuf, alisema School Pay imekuwa na mchango mkubwa katika kuweka kumbukumbu sahihi za malipo ya ada na kuwawezesha wazazi kupata risiti mara baada ya kufanya malipo.
Alisema mfumo huo pia umepunguza ulazima wa wazazi kufika shuleni kwa ajili ya kulipa ada au kufuatilia risiti, kwa kuwa wanaweza kukamilisha mchakato huo wakiwa nyumbani.
Naye mzazi wa mwanafunzi wa Salaam Pre and Primary School, Hassan Said Malipa, alisema mfumo huo umemsaidia yeye na wazazi wengine kufuatilia kwa urahisi kiasi cha ada kilicholipwa na salio lililobaki.
Malipa alisema uwezo wa kufanya malipo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa kipato umekuwa msaada mkubwa kwa wazazi, huku taarifa za malipo zikipatikana kwa wakati.
