×

Iran Yatoa Milioni 78 kwa Atakayeua au Kukamata Mwanajeshi wa Marekani, Mkuu wa Jeshi Afunguka

Mkuu wa Jeshi la Iran, Amir Hatami.

TEHRAN: Jeshi la Iran limetangaza zawadi ya Dola za Marekani 30,000, sawa na takribani Sh milioni 78 kwa viwango vya sasa vya ubadilishaji, kwa mtu atakayemuua au kumkamata na kumkabidhi mwanajeshi wa Marekani.

Mkuu wa Jeshi la Iran, Amir Hatami, ametangaza mpango huo akisema umeanzishwa baada ya kupokea maombi mengi kutoka kwa watu waliotaka kushiriki katika hatua hiyo.

Hatami amesema mtu yeyote atakayefanikiwa kumuua au kumkamata na kumkabidhi kwa mamlaka za Iran mwanajeshi wa Marekani atalipwa kiasi cha Dola 30,000, au takribani tomani bilioni tano.

Aidha, amesema wanawake wa Iran watakaotekeleza kitendo hicho watalipwa mara mbili, hivyo zawadi inaweza kufikia Dola 60,000.

Hata hivyo, Hatami hakueleza ni wapi wala lini wanajeshi wa Marekani wanaotarajiwa kulengwa watapatikana.

Tangazo hilo limekuja wakati mvutano kati ya Iran na Marekani ukiendelea, huku Tehran ikiendelea kuitaka Marekani kuondoka Mashariki ya Kati.

Hatami pia amesema vikosi vya Marekani havina ruhusa tena ya kuingia katika Ghuba ya Uajemi, Ghuba ya Oman na Mlango wa Bahari wa Hormuz, eneo ambalo ni muhimu kwa usafirishaji wa mafuta duniani.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa, hakuna uwepo unaojulikana wa vikosi vya ardhini vya Marekani ndani ya Iran, isipokuwa operesheni ya uokoaji iliyofanyika Aprili baada ya ndege ya Marekani kuanguka.

Mzozo huo umeendelea kuwa na athari katika eneo la Mashariki ya Kati, huku Iran na Marekani zikiendelea kubadilishana mashambulizi kwa vipindi na juhudi za kidiplomasia kupitia wapatanishi zikiwa bado hazijazaa matokeo makubwa.

Tangazo la Iran limeongeza wasiwasi kuhusu usalama wa wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo na linaweza kuongeza zaidi mvutano kati ya Tehran na Washington.

Leave a Comment