×

Trump Aongeza Shinikizo, Ataka Hormuz Kuwa “Eneo Jipya la Marekani”

Rais wa Marekani Donald Trump ameendelea kusisitiza tishio lake la kutaka Marekani ichukue mamlaka Mlango wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa nishati duniani, wakati vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran vikiendelea bila dalili za kumalizika hivi karibuni.

Kauli hiyo imekuja huku kukiwa na taarifa zinazokinzana kuhusu uwepo wa mazungumzo kati ya Washington na Tehran. Mjumbe wa Trump na mkwe wake, Jared Kushner, alisema Jumatatu kuwa Marekani na Iran zilikuwa zikifanya mazungumzo. Hata hivyo, Trump alikanusha taarifa hizo.

Kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump alisema hakuna mazungumzo yanayoendelea wala yaliyopangwa na Iran, huku akisisitiza kuwa kizuizi cha majini cha Marekani bado kinaendelea.

Trump pia alidai kuwa Mlango wa Hormuz uko wazi na unafanya kazi, na kwamba mabomu yote ya majini yaliyokuwa hatari katika eneo hilo yameondolewa au kulipuliwa.

Hata hivyo, vyanzo vya Marekani vilivyozungumza na AFP vilisema kulikuwa na mazungumzo chanya na upande wa Iran, lakini Trump ameamua kusubiri hadi Tehran iwe tayari kufikia makubaliano.

Jumanne, Trump alichapisha pia ramani kwenye Truth Social iliyouonyesha Mlango wa Hormuz kama eneo jipya la Marekani.  Hatua hiyo imeongeza wasiwasi kuhusu msimamo wa Washington katika mzozo huo.

Mlango wa Hormuz ni njia muhimu sana kwa uchumi wa dunia, kwani takribani moja ya tano ya mafuta yanayosafirishwa duniani hupitia eneo hilo.

Iran imesema haitafungua tena njia hiyo kikamilifu hadi Marekani itimize madai yake, ambayo ni pamoja na kuondoa vikwazo dhidi ya bandari za Iran, kuondoa baadhi ya vikwazo vya mafuta, kufungua mali za Iran zilizogandishwa na kulipa fidia kwa madhara ya vita.

Mjumbe mkuu wa Iran katika mazungumzo hayo, Mohammad Bagher Ghalibaf, amesema wazi kuwa Mlango wa Hormuz hautafunguliwa hadi masharti yaliyowekwa na Iran yatimizwe.

Wakati huohuo, mshirika wa Trump, Jared Kushner, amesema rais huyo yuko tayari kuwa mvumilivu na hataki kukimbilia makubaliano.

Qatar, ambayo imekuwa ikisaidia katika juhudi za upatanishi kati ya Marekani na Iran, imesema makubaliano kati ya Iran na Oman kuhusu Mlango wa Hormuz yanaweza kusaidia kurejesha mazungumzo ya kumaliza vita vya Mashariki ya Kati.

Mzozo huo pia umeongeza shinikizo la kisiasa kwa Trump, huku gharama za maisha nchini Marekani zikiongezeka na uchaguzi wa katikati ya muhula ukitarajiwa kufanyika mwezi Novemba.

Kwa sasa, juhudi za kidiplomasia zinaendelea, lakini msimamo mkali wa pande zote mbili unaendelea kufanya uwezekano wa makubaliano ya haraka kuwa mgumu.

Leave a Comment