×

Waziri wa Kilimo Zanzibar Apongeza Kasi ya Ujenzi wa Seed Farm na Mabwawa ya Umwagiliaji

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Suleiman Masoud Makame (katikati) akiongea na wafanyakazi wa kampuni ya Bluemark Real Estate Company Limited (BRECOL) alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Seed Farm, Farmer Centre, mabwawa ya umwagiliaji pamoja na maabara ya kisasa ya kilimo katika maeneo ya Mtwango, Kibonde Mzungu na Kizimbani.

Zanzibar. Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Suleiman Masoud Makame, amepongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya kilimo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Makame ametoa pongezi hizo baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Seed Farm, Farmer Centre, mabwawa ya umwagiliaji pamoja na maabara ya kisasa ya kilimo katika maeneo ya Mtwango, Kibonde Mzungu na Kizimbani.

Miradi hiyo inatekelezwa na kampuni ya Bluemark Real Estate Company Limited (BRECOL).

Waziri Makame amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi pamoja na kasi ambayo kampuni hiyo imeonyesha katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili ianze kutoa huduma zilizokusudiwa, ikiwemo kuongeza uzalishaji wa mbegu bora, kuboresha huduma za ugani, kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na kuongeza tija kwa wakulima.


“Matarajio yetu ni kuona miradi hii inakamilika kwa viwango vya hali ya juu na kuwa miongoni mwa miradi itakayozinduliwa wakati wa Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar,” amesema Makame.

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Suleiman Masoud Makame akiongea jambo.

Aidha, amewataka wasimamizi wa miradi na wakandarasi kuendelea kuongeza kasi ya utekelezaji, huku wakizingatia ubora wa kazi na viwango vya kitaalamu ili kuhakikisha Serikali inapata thamani halisi ya fedha zinazowekezwa.

Kwa upande wake, BRECOL imeendelea na utekelezaji wa miradi hiyo kwa kasi, ikiwa na lengo la kuhakikisha inakamilika ndani ya muda uliopangwa na kuchangia mageuzi katika sekta ya kilimo Zanzibar.

Ujenzi wa Seed Farm, Farmer Centre, maabara ya kisasa na mabwawa ya umwagiliaji ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu ya kilimo, kuongeza upatikanaji wa mbegu bora na kuboresha huduma za kitaalamu kwa wakulima.

Miradi hiyo pia inalenga kuchangia katika usalama wa chakula, kuongeza uzalishaji wa kilimo na kuimarisha uchumi wa Zanzibar.

Leave a Comment