×

Maharusi Wafariki Dunia Katika Ajali ya Helikopta Wakiwa Honeymoon

Maharusi Alexander Cromie na Marie Ebert wamefariki dunia pamoja na rubani wao katika ajali ya helikopta nchini Ugiriki.

Maharusi kutoka Uingereza wamefariki dunia pamoja na rubani wao katika ajali ya helikopta nchini Ugiriki, dakika chache kabla ya kutua katika eneo walilokuwa wakielekea.

Alexander Cromie na Marie Ebert walikuwa katika safari yao ya honeymoon katika kisiwa cha Sifnos, nchini Ugiriki, wakati helikopta waliyokuwa wakisafiria ilipoanguka katika eneo la Tholos Jumatatu, Agosti 17, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, helikopta hiyo ilianguka na kushika moto mkubwa, huku mabaki ya ndege hiyo yakitawanyika katika eneo la tukio.

Rubani aliyefariki ametajwa kuwa Giorgos Raikos, mwenye umri wa miaka 55, ambaye kwa mujibu wa taarifa alikuwa mwanajeshi mkongwe wa Jeshi la Ugiriki kabla ya kustaafu na kuendelea na kazi ya urubani wa helikopta.

Taarifa zinaeleza kuwa Maharusi hao walikuwa wakisafiri kuelekea Sifnos kutoka Markopoulo, eneo lililopo kusini-mashariki mwa Athens.

Ajali hiyo ilitokea dakika chache kabla ya muda uliopangwa wa kutua saa 12:15 jioni, huku helikopta hiyo ikiwa ilitarajiwa kuondoka tena baada ya dakika 25.

Mashuhuda walieleza kusikia sauti isiyo ya kawaida kutoka kwenye injini ya helikopta hiyo kabla haijaanguka.

Video iliyosambaa mitandaoni ilionyesha helikopta hiyo ikizunguka angani na kushuka kwa kasi kabla ya kugonga ardhi na kusababisha moto.

Marie Ebert

Wazima moto, madaktari na polisi waliwasili eneo la tukio muda mfupi baada ya ajali hiyo. Miili ya wahanga wote watatu ilipatikana katika eneo la ajali.

Mamlaka za usalama wa anga nchini Ugiriki zimeanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Wachunguzi wanatarajiwa kuchunguza rekodi za safari, hali ya hewa, mifumo ya helikopta na uwezekano wa hitilafu ya kiufundi.

Taarifa za awali zilisema hali ya hewa ilikuwa ya kawaida wakati wa tukio na hakukuwa na taarifa za upepo mkali.

Alexander Cromie

Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza imesema iko katika mawasiliano na mamlaka za Ugiriki na iko tayari kutoa msaada kwa familia za Cromie na Ebert.

Kifo cha Maharusi hao kimegeuza safari yao ya honeymoon kuwa msiba mkubwa, huku uchunguzi ukiendelea kubaini kilichosababisha helikopta hiyo kuanguka dakika chache tu kabla ya kufika walikokuwa wakielekea.

Leave a Comment