
Dar es Salaam. Meneja Mradi wa Taasisi ya Utamaduni na Maendeleo Afrika Mashariki (CDEA), Angela Kilusungu, amesema elimu ya hakimiliki ni muhimu kwa wanamuziki, watayarishaji, watunzi na wadau wengine wa sekta ya muziki ili waweze kulinda na kunufaika na kazi zao, hususani zinapotumika katika matamasha na mashindano makubwa ya michezo.
Akizungumza leo katika Jukwaa la Mashariki la Creative Economy Expo 2026 linalofanyika Mlimani City, Dar es Salaam, Kilusungu amesema siku ya tatu ya maonyesho hayo imejikita katika sekta ya muziki, ambapo washiriki wanapatiwa elimu kuhusu namna ya kulinda haki zao za kazi za muziki katika majukwaa mbalimbali.
Amesema Tanzania pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaendelea kujiandaa kwa mashindano makubwa ya soka, hivyo ni muhimu wanamuziki kufahamu namna kazi zao zinavyoweza kutumika katika michuano hiyo bila kupoteza haki zao.

“Mwanamuziki akijua haki yake, anajua namna ya kuitumia na kuilinda kwenye majukwaa mbalimbali,” amesema Kilusungu.
Kwa mujibu wa Kilusungu, mafunzo hayo yanawalenga zaidi wanamuziki, producers, composers na wadau wengine wanaomiliki haki katika mnyororo wa thamani wa muziki.
Amesema moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele ni elimu kuhusu Copyright Friendly Label, ambayo inalenga kusaidia wadau kuelewa namna ya kutumia mfumo huo katika matamasha makubwa na mashindano ya michezo, ikiwemo kandanda.

Aidha, amesema CDEA imetenga siku zote nne za Mashariki Creative Economy Expo kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria wa hakimiliki bure, kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni, kwa wabunifu na wadau wanaohitaji ushauri kuhusu hakimiliki na mikataba.
Kwa Upande wao wasanii wa muziki walioshiriki Katika Jukwaa hilo Jordan Wilson na Masoud Kandoro wamesema wamejifunza Haki Miliki na namna gani wataandaa kazi zilizo Bora ukilinganisha na kipindi Cha nyuma kabla hawajapata Mafunzo hayo