
Wakili wa kujitegemea Peter Madeleka amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka matano ya kudharau mahakama.
Madeleka amesomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Hassan Makube. Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu Job Mrema, Wakili wa Serikali Mwandamizi Clemence Kato pamoja na Moseie Kaima na Veronica Chacha, huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Maduhu William.
Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali Kato, mashtaka hayo yanahusiana na kauli na taarifa ambazo Madeleka anadaiwa kutoa au kuchapisha kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, ikiwemo Jambo TV, kuhusu kesi ya uhujumu uchumi namba 4521/2026 inayomkabili Wendy Ishengoma na wenzake wanne katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Makosa ya Uhujumu Uchumi.
Jamhuri inadai kuwa Julai 27 na 28, 2026, akiwa maeneo ya Mawasiliano, Ubungo, Madeleka alitoa taarifa kuhusu kesi hiyo wakati akiwa wakili wa utetezi, jambo linalodaiwa kukiuka amri ya Mahakama iliyotolewa Julai 27, 2026.

Aidha, anadaiwa kufanya kitendo kama hicho Agosti 7, 2026, akiwa Mikocheni, Kinondoni, kwa kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa kesi hiyo kupitia vyombo vya habari.
Katika shtaka jingine, Madeleka anadaiwa kutoa kauli iliyodaiwa kupotosha mwenendo wa kesi, ikiwemo madai kwamba “Mawakili wa Serikali walikuwa wanaomba vielelezo vilivyotolewa mahakamani vikahifadhiwe kwenye Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,” huku Jamhuri ikidai kuwa alijua kauli hiyo haikuwa ya kweli.
Shtaka la mwisho linahusu tukio la Agosti 13, 2026, ambapo anadaiwa tena kutoa na kuchapisha taarifa kuhusu kesi hiyo, kitendo ambacho Jamhuri inadai kilikiuka amri ya Mahakama ya Julai 27, 2026.
Madeleka amekana mashtaka yote akisema tuhuma hizo si za kweli.
Ameachiwa kwa dhamana baada ya kuwa na wadhamini wawili waliotia saini bondi ya Shilingi milioni tano kila mmoja. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 9, 2026