
BERLIN, Ujerumani — Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga, inajiandaa kufungua msimu mpya wa 2026/27 Agosti 28, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona ushindani katika mbio za kuwania ubingwa, nafasi za michuano ya Ulaya pamoja na mapambano ya kuepuka kushuka daraja.
Msimu huo utafunguliwa rasmi Ijumaa, Agosti 28, kwa mabingwa watetezi Bayern Munich kuanza kampeni yao mbele ya mashabiki wao dhidi ya VfB Stuttgart.
Mchezo huo utachezwa katika Uwanja wa Allianz Arena kuanzia saa 21:30, huku Bayern ikitarajiwa kuanza safari ya kutetea taji lake kwa kutafuta pointi tatu za mwanzo.
Mechi Sita Jumamosi
Jumamosi, Agosti 29, kutakuwa na michezo sita katika ratiba ya Bundesliga.
SV Elversberg itakuwa mwenyeji wa Bayer Leverkusen katika Uwanja wa Ursapharm-Arena an der Kaiserlinde, huku mchezo huo ukipangwa kuanza saa 16:30.
Wakati huo huo, FC Köln itakuwa nyumbani dhidi ya Hoffenheim katika Uwanja wa RheinEnergieSTADION kuanzia saa 16:30.
Mchezo mwingine utawakutanisha Mainz na Paderborn katika Uwanja wa MEWA ARENA, pia kuanzia saa 16:30.
RB Leipzig nayo itaanza msimu nyumbani dhidi ya Borussia Mönchengladbach katika Uwanja wa Red Bull Arena. Mchezo huo umepangwa kuanza saa 16:30.
Katika mchezo mwingine wa muda huo, Union Berlin itakuwa mwenyeji wa Eintracht Frankfurt katika Uwanja wa Stadion An der Alten Försterei.
Dortmund Kuanzia Nyumbani
Mchezo wa mwisho wa Jumamosi utawakutanisha Borussia Dortmund na Hamburger SV katika Uwanja wa Signal Iduna Park.
Dortmund itakuwa mwenyeji katika mchezo huo unaotarajiwa kuanza saa 19:30, huku mashabiki wakisubiri kuona namna timu hiyo itakavyoanza msimu mpya.
Michezo Miwili Jumapili
Ratiba ya wiki ya kwanza itahitimishwa Jumapili, Agosti 30, kwa michezo miwili.
Freiburg itakuwa mwenyeji wa Werder Bremen katika Uwanja wa Europa-Park Stadion kuanzia saa 16:30.
Baadaye, Augsburg itakutana na Schalke katika Uwanja wa WWK ARENA kuanzia saa 18:30.
Msimu Mpya Waanza kwa Kishindo
Kwa ujumla, msimu mpya wa Bundesliga unatarajiwa kuanza kwa ushindani mkubwa huku kila timu ikiwa na malengo yake.
Macho mengi yataelekezwa kwa Bayern Munich, ambayo itaanza kampeni ya kutetea ubingwa mbele ya Stuttgart, lakini ushindani kutoka kwa Dortmund, Leipzig, Leverkusen na timu nyingine unatarajiwa kufanya mbio za msimu huu kuwa na mvuto mkubwa.
Mashabiki wa Bundesliga sasa wanasubiri Agosti 28 ifike ili kuona pazia la msimu mpya likifunguliwa rasmi.
Stori na Haika Urio | GPL – TUDACO