×

Expo Yawafundisha Waandishi Jinsi ya Kulinda na Kuthamini Kazi Zao

Meneja Mradi katika Taasisi ya Utamaduni na Maendeleo Afrika Mashariki, Anjela Kilusungu, amesema Mashariki Creative Economy Expo 2026 imekuwa jukwaa muhimu la kutoa elimu kwa waandishi na wachapishaji kuhusu umuhimu wa kulinda kazi zao za ubunifu.

Akizungumza katika siku ya mwisho ya expo hiyo, Kilusungu amesema tukio hilo limewapa wadau wa sekta ya ubunifu nafasi ya kuelewa zaidi thamani ya kazi zao, pamoja na namna ya kuzilinda dhidi ya matumizi yasiyo halali.

Amesema kazi za ubunifu zina thamani kubwa kiuchumi, hivyo waandishi na wachapishaji wanapaswa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu haki zao za ubunifu na namna ya kuzitumia kazi hizo kama chanzo cha kipato.

Kwa mujibu wa Kilusungu, elimu hiyo ni muhimu katika kuwasaidia wabunifu kutambua kuwa kazi wanazozalisha si kwa ajili ya burudani pekee, bali pia zinaweza kuwa sehemu ya kujenga mafanikio na kipato endelevu.

Ameongeza kuwa kupitia expo hiyo, wadau wamepata nafasi ya kujifunza namna ya kutambua thamani ya kazi zao na kuchukua hatua za kuzilinda ili zisitumike bila idhini au kunufaisha watu wengine bila kuwahusisha wenye kazi hizo.

Kilusungu amesisitiza umuhimu wa waandishi na wachapishaji kujenga uelewa kuhusu haki zao, ili waweze kutumia fursa zinazotokana na uchumi wa ubunifu na kuhakikisha kazi zao zinawanufaisha kiuchumi.

Mashariki Creative Economy Expo 2026 imewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya ubunifu kwa lengo la kubadilishana maarifa, kujenga mitandao na kuangalia fursa zinazoweza kuchochea ukuaji wa uchumi wa ubunifu.

Leave a Comment