
Mwanamuziki mkongwe wa Tanzania, Lady Jaydee, leo Ijumaa, Agosti 21, 2026, ameachia rasmi wimbo wake mpya unaoitwa “Pressure”, unaopatikana kwenye majukwaa mbalimbali ya kusikiliza muziki.
Kupitia wimbo huo, Lady Jaydee anaelezea hali ya mtu aliye katika uhusiano wa kimapenzi huku akihisi kuwa mwenza wake hamwamini.
Licha ya kuona dalili za kutokuaminiana katika uhusiano huo, mhusika anajikuta akishindwa kuondoka kutokana na hisia za mapenzi ambazo bado zinamfanya atamani kuendelea kubaki.
“Pressure” unaangazia kwa kina mgongano upendo, hisia na kujilinda dhidi ya maumivu ya kimapenzi, hali ambayo watu wengi wanaweza kujikuta wakipitia katika mahusiano yao.
Wimbo huo unalenga kuwagusa watu ambao wakati mwingine akili huwaambia waondoke kwenye uhusiano usiowapa amani, lakini moyo bado huwalazimisha kubaki.
Lady Jaydee ni miongoni mwa wasanii wenye historia kubwa katika muziki wa Bongo Flava, akiwa na safari ya zaidi ya miongo miwili katika tasnia ya muziki Tanzania.
Kutolewa kwa “Pressure” kunaongeza kazi mpya katika orodha ya nyimbo za msanii huyo, huku mashabiki wake wakiwa na fursa ya kuusikiliza kuanzia leo, Agosti 21, 2026, kupitia majukwaa mbalimbali ya muziki.
Stori na Ashura Karimu | GPL – TUDACO