
Nyota wa Inter Miami, Lionel Messi, ameadhibiwa kwa faini na Ligi Kuu ya Soka Marekani (MLS) kufuatia tukio la kumpiga kwa mkono eneo la shingo na kichwa mchezaji wa Philadelphia Union, Quinn Sullivan.
Tukio hilo lilitokea katika dakika za nyongeza za mchezo wa Agosti 19, 2026, uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 kati ya Philadelphia Union na Inter Miami.
Messi na Sullivan walikuwa wakibishana wakati nyota huyo wa Argentina alipoonekana kumpiga Sullivan katika eneo la nyuma ya shingo na kichwa. Mwamuzi hakutoa kadi kwa Messi wakati tukio hilo lilipotokea.
Baada ya mchezo, Kamati ya Nidhamu ya MLS ilichunguza tukio hilo na kuamua kumtoza Messi faini.
MLS haikufichua kiasi cha fedha ambacho Messi anatakiwa kulipa, lakini ilieleza kuwa adhabu hiyo imetokana na kanuni zinazowakataza wachezaji kuweka mikono kwenye uso, kichwa au shingo ya mpinzani.
Pamoja na adhabu hiyo, Messi hatakosa michezo yoyote kutokana na tukio hilo, kwani MLS haikumpa adhabu ya kusimamishwa.
Mchezaji wa Inter Miami, Ian Fray, pia alitozwa faini kutokana na tukio tofauti lililotokea katika mchezo huo, huku kadi nyekundu aliyoonyeshwa Cavan Sullivan wa Philadelphia Union baadaye ikiondolewa baada ya rufaa.
Tukio hilo limeibua mjadala kuhusu nidhamu ya Messi ndani ya uwanja, licha ya kuendelea kuwa mchezaji muhimu wa Inter Miami.
Katika mchezo huo, Messi alifunga bao moja na kutoa pasi ya bao, lakini Inter Miami ililazimika kuridhika na sare ya mabao 2-2.
Stori Na Erick Elibariki