×

Tundu Lissu Afunguka Hadharani; Nimepigania Haki Tangu Nikiwa Shuleni

Ikiwa ni mwendelezo wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ambaye sasa anajitetea mwenyewe katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Kanda ya Dar es Salaam, Lissu amefunguka namna ambavyo mchakato wa “No Reform, No Election” ulivyoanzia ndani ya chama, akieleza kuwa msimamo huo haukuwa kauli yake binafsi, bali ulikuwa msimamo wa CHADEMA ulioanzia katika maamuzi ya chama kabla ya uchaguzi wa ndani wa uongozi.

Lissu amesema kuwa tarehe 10 Desemba 2024, Mwenyekiti wa wakati huo wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ndiye aliyetamka msimamo huo, huku chama kikisubiri kwanza uchaguzi wake wa ndani uliokuwa umepangwa kufanyika Januari 2025.

Lissu amesema kuwa tarehe 20 Januari 2025, Baraza Kuu la CHADEMA lilifanya kikao chake, ambacho kwa mujibu wa utaratibu wa chama ndicho chombo kinachopokea na kupendekeza ajenda zitakazojadiliwa katika Mkutano Mkuu. Aidha, amesema kuwa Kamati Kuu iliwasilisha mapendekezo kuhusu msimamo wa “No Reform, No Election” kwa Baraza Kuu, na baada ya kukubaliwa, suala hilo likapendekezwa kuwa ajenda ya Mkutano Mkuu wa chama uliofanyika Januari 21, 2025.

Katika Mkutano huo Mkuu, Lissu amesema, pamoja na masuala mengine ya chama, mambo mawili muhimu yalifanyika. Kwanza, ulipitishwa msimamo wa CHADEMA kuhusu “No Reform, No Election”, na pili, uchaguzi wa viongozi wa chama ulifanyika ambapo yeye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA. Vilevile, Lissu amesema kuwa baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti, alimteua John Mnyika kuwa Katibu Mkuu, huku Golugwa akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara na kiongozi mwingine akiteuliwa kwa upande wa Zanzibar.

Baada ya uongozi huo mpya kuingia madarakani, Lissu amesema kuwa walianza maandalizi ya mkakati wa “No Reform, No Election”, ambao ulikuwa na lengo la kuhamasisha wananchi nchini kuhusu masuala ya demokrasia na mabadiliko ya kisiasa.

Amesema kuwa mpango huo haukuwa wa kupanga kufanya uhaini, kuchoma nyumba za watu au kuvunja sheria za nchi, bali ulikuwa wa kuhamasisha umma na kuwasisitiza wananchi kudai mabadiliko ya kisiasa kwa njia za kisiasa, ikiwemo mikutano na maandamano.

Aidha, Lissu amesema kuwa katika utekelezaji wa mkakati huo, walipanga kuzungumza na Watanzania kupitia makundi na taasisi mbalimbali katika maeneo yao. Amesema miongoni mwa taasisi walizoanza nazo zilikuwa taasisi za kidini, ambapo walianza na shula za maimamu.

Hata hivyo, amesema hawakuhusika na BAKWATA wala CCM. Pia, amesema waliomba kukutana na Baraza la Maaskofu, lakini hawakufanikiwa kukutana nao, huku wakifanikiwa kukutana na Jukwaa la Wahariri wa vyombo vya habari na kuzungumza nao kuhusu masuala hayo.

Vilevile, Lissu amesema kuwa kwa kuwa Tanzania ina uhusiano na marafiki katika nchi nyingine, waliamua kwenda Nairobi na kukutana na Raila Odinga, ambaye wakati huo alikuwa hai, pamoja na kwenda kumuona Mzee Warioba ili kuzungumza naye kuhusu “No Reform, No Election” na msimamo wao wa kisiasa.

Aidha, amesema kuwa alialikwa katika Chuo Kikuu cha Makerere kuzungumza kuhusu Mwalimu Julius Nyerere na urithi wake, na katika mazungumzo hayo alizungumzia pia changamoto za mfumo wa kikatiba nchini.
Lissu amesema kuwa baada ya kurejea nchini, majukumu yaligawanywa kwa ajili ya kuanza ziara mbalimbali.

Amesema yeye alipangiwa Kanda ya Nyasa, ambako alipaswa kuzungumza katika mikutano ya hadhara. Lissu amesisitiza kuwa katika ziara hizo hawakuwa wanapanga kufanya uhaini wala kuvunja sheria za nchi.

Amesema ziara yao ya kwanza waliimaliza Iringa tarehe 30 Machi 2025. Baada ya hapo, Naibu Katibu Mkuu Golugwa alimtumia ujumbe mfupi wa simu akimtaka kuandaa watia nia kwa ajili ya uchaguzi mkuu. Pia, amesema alitumiwa ujumbe kwamba tarehe 3 Aprili 2025 alitakiwa kufika Makao Makuu ya chama kwa ajili ya kuzungumza na watia nia hao kuhusu msimamo wa chama.

Lissu amesema tarehe 1 Aprili alirejea Dar es Salaam akiwa pamoja na John Heche kwa ajili ya maandalizi ya mkutano huo. Amesema mkutano huo uliofanyika kwa lengo la kuzungumza na watia nia na kuwaeleza msimamo wa CHADEMA kama chama.

Lissu amesema yeye ndiye alikuwa mzungumzaji katika mkutano huo, na kwamba hilo lilikuwa jukumu lake la kuzungumza baada ya mkutano kuandaliwa na taarifa kutolewa na Katibu Mkuu.
Kwa msingi huo, Lissu amesema anashangaa kusikia kwamba yeye ndiye aliyeandaa mkutano huo. Amesema kama wangeuliza ni nani aliyeuandaa, wangeweza kupata majibu kuhusu mtu aliyekuwa na jukumu hilo.

Aidha, amesema yeye alipewa taarifa na Katibu Mkuu kuhusu jukumu lake la kwenda kuzungumza katika mkutano huo, hivyo kuwa mzungumzaji hakumaanishi kwamba ndiye aliyekuwa mratibu au mwandaaji wa mkutano.

Lissu amesema ushahidi uliowasilishwa mahakamani na mashahidi 17 pia unaibua maswali. Amesema kuna maneno katika ushahidi huo ambayo, ukisoma tu, hayangeweza hata kuchukua dakika moja, wakati mkutano wake ulikuwa mrefu sana. Kuhusu video ambayo anadaiwa kuichapisha kupitia Jambo TV, Lissu amesema hajawahi kuiona hadi leo.

Kwa hiyo, amesema akiulizwa alitumia dakika ngapi kwenye video hiyo, hawezi kutoa jibu kwa sababu hajawahi kuiona.
Lissu amesema siku hiyo ya mkutano aliulizwa maswali mengi na alijibu maswali yote, akisisitiza kuwa mkutano huo ulikuwa wa zaidi ya saa tatu.

Aidha, amesema hakufanikiwa kuiona video hiyo kwa sababu kesho yake, tarehe 4 Aprili 2025, walielekea katika ziara mkoani Ruvuma.

Amesema tarehe 9 Aprili 2025, alipokuwa akielekea kumaliza mkutano wake jioni huko Mbinga, alikamatwa na kupigwa kabla ya kupelekwa katika kituo cha polisi Mbinga. Baadaye, amesema alihamishiwa Songea mjini, katika ofisi ya RPC.

Akiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi, Lissu amesema alieleza kuwa alikuwa na njaa na kuwaambia polisi kwamba alikuwa na dada yake katika eneo hilo ambaye angeweza kumletea chakula. Amesema majira ya saa nne usiku chakula kilifika na baadaye usiku alipelekwa Dar es Salaam.
Lissu amesema kwa mtazamo wake, shahidi pekee aliyesema ukweli ni P17, huku akidai mashahidi wengine walitoa maelezo ambayo hayakuwa sahihi.

Amesema P17 ndiye aliyesema kuwa yeye ndiye aliyekuwa amechapisha maudhui hayo mtandaoni, siyo Lissu. Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, Lissu amesema P17 alipata taarifa kutoka kwa bosi wake, John Marwa, ambaye naye alikuwa amepewa taarifa na Ofisa Habari wa chama, Brenda Rupia.
Hapo ndipo Lissu anapoona mkanganyiko mkubwa katika upande wa mashtaka.

Amesema upande wa mashtaka unamhusisha yeye na uchapishaji wa maudhui hayo mtandaoni, wakati wao wenyewe walimleta P17 kama shahidi na P17 akaeleza kuwa yeye ndiye aliyerusha maudhui hayo mtandaoni.
Vilevile, Lissu amesema upande wa mashtaka unadai kuwa yeye ndiye aliyeandaa mkutano, wakati kwa maelezo yake yeye alikuwa mzungumzaji tu na mkutano uliandaliwa na chama, huku taarifa kuhusu kushiriki kwake akipewa na Katibu Mkuu.

Kwa hiyo, Lissu amesema kama kweli kulikuwa na mtu aliyekuwa na jukumu la kuandaa mkutano huo, ushahidi ulipaswa kuelekeza kwa mhusika aliyekuwa na jukumu hilo, badala ya kumhusisha yeye kwa sababu tu alikuwa mzungumzaji wa mkutano.

Leave a Comment