
Ohio, Marekani — Mmoja wa wamiliki wa klabu za Leeds United na Rangers, Jed York, amehukumiwa kifungo cha siku moja gerezani nchini Marekani baada ya kukamatwa katika operesheni ya polisi iliyohusisha tuhuma za ukahaba.
York, ambaye pia ni mmiliki mkuu wa timu ya NFL ya San Francisco 49ers, alikamatwa Jumapili, Agosti 23, katika eneo la East Palestine, Ohio, wakati wa operesheni iliyofanywa na polisi kwa kushirikiana na Mahoning Valley Human Trafficking Task Force.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, York alidaiwa kujibu tangazo la siri lililowekwa mtandaoni na maafisa waliokuwa wakifanya uchunguzi. Inadaiwa alipanga kulipa dola 140 kwa ajili ya kufanya tendo la ngono.
Awali, York alishtakiwa kwa kosa la kujihusisha na ukahaba. Hata hivyo, waendesha mashtaka baadaye walibadilisha shtaka hilo na kuwa tabia isiyo na nidhamu (disorderly conduct). Pia alishtakiwa kwa kumiliki chombo kilichotumika katika kutenda kosa, huku simu yake ikitajwa kuwa ilitumika kuwasiliana na tangazo hilo.
York alikubali no contest katika mahakama ya Ohio, hatua ambayo si kukiri rasmi hatia, lakini inamruhusu mahakama kutoa hukumu.
Mahakama ilimhukumu kifungo cha siku moja kwa kila kosa, huku vifungo hivyo vikienda kwa wakati mmoja. Muda aliokuwa tayari ameshikiliwa ulihesabiwa kama sehemu ya adhabu hiyo.
Mbali na kifungo hicho, York alitozwa faini ya dola 1,150. Pia alitakiwa kukamilisha kozi ya mtandaoni, huku dola 160 zikielekezwa kwa Mahoning Valley Human Trafficking Task Force.
Baada ya kukamatwa, York aliachiliwa kwa dhamana ya dola 5,000 kabla ya kurejea mahakamani kukamilisha mchakato wa kesi.
Tukio hilo limeibua maswali kuhusu mustakabali wa York katika michezo, hasa kutokana na nafasi yake kama mmiliki wa timu ya San Francisco 49ers. NFL imesema inalifahamu suala hilo na italipitia kwa kuzingatia sera yake ya mwenendo binafsi inayowahusu pia wamiliki wa timu.
Katika soka la Uingereza na Scotland, York ni sehemu ya umiliki wa Leeds United na Rangers kupitia maslahi yanayohusishwa na 49ers Enterprises. Hadi sasa, klabu hizo hazijatoa kauli ya kina kuhusu tukio hilo.
Hata hivyo, York hakuhukumiwa kwa shtaka la ukahaba lenyewe baada ya shtaka hilo kubadilishwa. Alikubali mashtaka mawili madogo, akahukumiwa kifungo cha siku moja kilichohesabiwa kama muda aliokuwa tayari ameshikiliwa, na kutozwa faini ya dola 1,150.
Stori na Erick Elibariki | GPL – TUDACO