×

Stanbic Yaleta Mapinduzi ya Malipo kwa Wafanyabiashara Wanaoagiza China

Dar es Salaam, Agosti 27, 2026 — Wafanyabiashara wa Tanzania wanaofanya biashara na China sasa wanaweza kufanya malipo kwa wazabuni wao kwa kutumia Shilingi ya Tanzania moja kwa moja kwenda Yuan ya China, bila kupitia Dola ya Marekani kama ilivyokuwa ikifanyika hapo awali.

Huduma hiyo imekuwa miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele katika Jukwaa la Biashara Tanzania na China lililoandaliwa na Stanbic Bank Tanzania katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Jukwaa hilo limewakutanisha wafanyabiashara kutoka Tanzania, wawakilishi wa kampuni za China pamoja na taasisi za serikali na sekta binafsi, kwa lengo la kujadili namna ya kuongeza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China.

Shilingi kwenda Yuan moja kwa moja

Mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Lulu Kheri, amesema huduma hiyo inaweza kuwasaidia wafanyabiashara kupunguza gharama zinazotokana na kubadilisha fedha na changamoto za mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji.
“Kinachotuhusu sisi wafanyabiashara ni kiwango cha kubadilisha fedha, gharama na uhakika kwamba mzabuni wetu atapokea malipo yake. Huduma hii inarahisisha mchakato na inaweza kusaidia kulinda faida yetu,” amesema Kheri.

Huduma ya malipo ya moja kwa moja kutoka Shilingi kwenda Yuan, iliyozinduliwa Agosti 12, 2026, inawezeshwa kupitia mfumo wa Cross-Border Interbank Payment System (CIPS).

Mfumo huo unaondoa hatua ya ziada ya kubadilisha Shilingi kuwa Dola ya Marekani kabla ya fedha hizo kubadilishwa kwenda Yuan, hivyo kulenga kupunguza gharama na kurahisisha mchakato wa malipo kwa wafanyabiashara.

Stanbic: Tunawasaidia wafanyabiashara kuokoa gharama

Fredrick Max, Mkuu wa Idara ya Biashara wa Stanbic Bank Tanzania, amesema huduma hiyo imekuja kutatua changamoto ambayo wafanyabiashara wanaofanya biashara na China wamekuwa wakikabiliana nayo kwa muda mrefu.
“Kwa muda mrefu, wafanyabiashara walilazimika kubadilisha Shilingi kuwa Dola za Marekani na baadaye kuwa Yuan. Huduma yetu ya moja kwa moja ya Shilingi kwa Yuan inaondoa hatua hiyo ya ziada, na kuwasaidia wateja kuokoa muda, kusimamia gharama na kufanya miamala kwa ufanisi zaidi,” amesema Max.

Amesema kupitia mtandao wa Standard Bank Group pamoja na ushirikiano wa kimkakati na Industrial and Commercial Bank of China (ICBC), Stanbic pia inawawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kupata fursa za biashara na wazabuni pamoja na wanunuzi nchini China.

Tanzania yatakiwa kuongeza bidhaa zenye thamani

Katika mjadala wa jukwaa hilo, Alfred Ngelula, Mkuu wa Dawati la China kutoka TISEZA, amesema kupunguza gharama za kubadilisha Yuan na Shilingi kunaweza kuongeza ushindani wa Tanzania katika kuvutia wawekezaji kutoka China.

Kwa upande wake, Benson Nkini, Afisa Biashara Mwandamizi wa Tanzania Trade Development Authority (TanTrade), amesisitiza umuhimu wa Tanzania kuongeza mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani katika soko la China.

Amesema hatua hiyo itasaidia Tanzania kuongeza manufaa yatokanayo na biashara na soko hilo kubwa la kimataifa.

Stanbic yaendeleza ushiriki China

Stanbic Bank Tanzania pia imeendelea kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na fursa katika soko la China, ikiwapeleka wateja wake kushiriki katika China International Import Expo (CIIE) kwa miaka minne mfululizo.

Maonesho yajayo yanatarajiwa kufanyika Novemba 2026, yakitoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kukutana na wanunuzi, wazalishaji na washirika mbalimbali wa biashara kutoka China.

Kwa sasa, wafanyabiashara wanaweza kupata huduma ya malipo ya moja kwa moja ya Shilingi kwenda Yuan kupitia matawi ya Stanbic Bank Tanzania, huku wateja waliopo wakiwa na uwezekano wa kutumia njia za kidijitali baada ya kukamilisha taratibu zinazohitajika.

Leave a Comment