
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imempa mwanafunzi wa chuo mwenye umri wa miaka 18 adhabu ya miezi 12 kwa kosa la kusababisha kifo cha kichanga baada ya kujifungua.
Mahakama hiyo imempa mshtakiwa huyo masharti ya kutotenda kosa lolote, kuwa na mwenendo mzuri na kuripoti kila mwezi katika Kituo cha Polisi Chang’ombe, Temeke, kwa kipindi cha miezi 12.
Adhabu hiyo imetolewa, Agosti 31, 2026, na Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, chini ya Jaji Mkwizu.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kesi hiyo, Wakili wa Serikali, Amedeus Malya, amesema mshtakiwa alikuwa akikabiliwa na kesi ya jinai ya Jamhuri dhidi yake, iliyohusu kosa la kusababisha kifo cha kichanga na kukitupa chooni, kosa linalojulikana kama Infanticide.
Malya amesema shtaka hilo lilikuwa chini ya Kifungu cha 199 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Sura ya 16, kama ilivyorekebishwa mwaka 2023.

TUKIO LA NOVEMBA 2025
Kwa mujibu wa maelezo ya kesi hiyo, tukio hilo lilitokea Novemba 11, 2025, katika eneo la Mambo Street, Temeke, Dar es Salaam.
Mshtakiwa, ambaye alikuwa mama wa kichanga hicho, alidaiwa kujifungua mtoto wa kiume.
Mahakama ilielezwa kuwa wakati wa tukio hilo, mshtakiwa alikuwa bado hajapona kikamilifu kutokana na kujifungua, huku hali yake ya akili ikiwa imevurugika kufuatia uzazi huo.
Baada ya kujifungua, alidaiwa kufanya vitendo vilivyosababisha mtoto huyo kupoteza maisha.
Mtoto huyo aligundulika na kupelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu, lakini licha ya juhudi zilizofanywa na madaktari, alifariki dunia.
MWILI WAFANYIWA POST-MORTEM
Baada ya mtoto huyo kufariki, mwili wake ulipelekwa kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu (post-mortem) ili kubaini chanzo na mazingira ya kifo chake.
Jeshi la Polisi liliendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo na baadaye mshtakiwa alikamatwa na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.
Mshtakiwa alifikishwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, na kukabiliwa na shtaka la kusababisha kifo cha kichanga.
Baada ya mwenendo wa kesi hiyo, Mahakama imetoa adhabu ya miezi 12 chini ya masharti ya kutotenda kosa lolote, kuwa na mwenendo mzuri na kuripoti kila mwezi katika Kituo cha Polisi Chang’ombe, Temeke.