
MWIMBAJI maarufu wa Marekani, Beyoncé, Septemba 4, 2026, anatimiza miaka 45 huku akisherehekea safari yake ya maisha na familia yake, hususan watoto wake watatu, Blue Ivy, Rumi na Sir.
Beyoncé, ambaye ni mshindi wa tuzo mbalimbali za Grammy na mtayarishaji wa vibao vingi vilivyofanya vizuri duniani, amekuwa akilinda kwa kiasi kikubwa maisha yake binafsi pamoja na familia yake.
Hata hivyo, katika miaka mbalimbali amekuwa akiwapa mashabiki wake fursa ya kuona baadhi ya nyakati zake za furaha akiwa na watoto wake, ambao amewapata pamoja na mume wake, mwanamuziki Jay-Z.

Moja ya kumbukumbu zilizowahi kuvutia mashabiki ni picha ya Beyoncé akiwa amewabeba mapacha wake, Rumi na Sir, katika picha iliyopigwa wakati wa Halloween na baadaye kushirikishwa katika kusherehekea siku yake ya kuzaliwa mwaka 2019.
Beyoncé pia amekuwa akionekana mara kwa mara akiwa na mtoto wake mkubwa, Blue Ivy, katika matukio mbalimbali ya kimataifa. Miongoni mwa matukio hayo ni mahudhurio yao kwenye uzinduzi wa filamu The Lion King jijini Hollywood mwaka 2019, ambapo mama na mwana walionekana wakiwa wamevalia mavazi yenye rangi nyeusi na fedha.

Familia hiyo pia imewahi kuonekana pamoja katika michezo ya NBA na hafla za tuzo za Grammy. Mwaka 2018, Beyoncé, Blue Ivy na mama yake Beyoncé, Tina Knowles, walihudhuria mchezo wa NBA All-Star mjini Los Angeles.
Katika Tuzo za Grammy za mwaka huo, Blue Ivy alivutia umakini baada ya kuonekana akiwaashiria wazazi wake wapunguze shangwe wakati wa hotuba, tukio lililoenea sana mitandaoni.
Beyoncé pia amewahi kuwashirikisha watoto wake katika safari zake. Katika makala maalumu Beyoncé Presents: Making The Gift ya mwaka 2019, mashabiki walipata nafasi ya kuwaona Beyoncé na Jay-Z wakiwa pamoja na watoto wao wakati wa safari barani Afrika.

Beyoncé alisema wakati huo kuwa kutembelea nchi za Afrika kwake kulikuwa jambo la kihisia, akieleza umuhimu wa watoto wake kufahamu asili na historia yao.
Mwaka 2023, Blue Ivy alianza kuonekana jukwaani akiwa na mama yake katika ziara ya Renaissance World Tour. Akiwa na umri wa miaka 11, Blue Ivy alisafiri katika maeneo mbalimbali duniani na kuendelea kuonyesha uwezo wake wa kucheza, hatua iliyomjengea umaarufu wake mwenyewe miongoni mwa mashabiki.
Safari hiyo pia ilionyeshwa katika filamu ya tamasha, Renaissance: A Film by Beyoncé, iliyowapa mashabiki picha za nyuma ya pazia za ziara hiyo.

Mwaka 2024, Beyoncé na Blue Ivy walionekana pamoja katika Tuzo za Grammy, kabla ya wawili hao kuonekana tena katika uzinduzi wa filamu Mufasa: The Lion King. Katika filamu hiyo, Blue Ivy alitoa sauti ya mhusika Kiara, binti wa Simba na Nala, ikiwa ni moja ya hatua kubwa katika safari yake ya kisanii.
Katika Tuzo za Grammy za mwaka 2025, Blue Ivy alisimama karibu na mama yake wakati Beyoncé akiweka historia kwa kushinda tuzo yake ya kwanza ya Album of the Year.

Familia hiyo iliendelea kuonekana pamoja katika Cowboy Carter Tour, ambapo Beyoncé aliwasogeza karibu watoto wake. Katika ziara hiyo, Rumi naye alipata nafasi ya kwanza kuonekana jukwaani katika uwanja mkubwa, akiambatana na mama yake na dada yake Blue Ivy wakati wa kuimba wimbo Protector.
Hivi karibuni, Blue Ivy pia aliungana na wazazi wake katika Met Gala ya mwaka 2026, akiwa amevalia gauni la Balenciaga pamoja na koti linaloendana nalo.
Beyoncé alisema wakati wa tukio hilo kuwa ilikuwa hisia za kipekee kwake kumuona binti yake akiwa sehemu ya tukio hilo kubwa la mitindo.
Katika kutimiza miaka 45, safari ya Beyoncé inaendelea kuonyesha si tu mafanikio yake katika muziki, bali pia nafasi kubwa ambayo familia yake imekuwa nayo katika maisha na kazi yake ya kisanii.