
Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo, Septemba 4, 2026 ameongoza jopo la madiwani na wataalamu kutoka Halmashauri ya Buchosa katika ziara ya mafunzo jijini Dodoma, kwa lengo la kujifunza namna Halmashauri ya Jiji la Dodoma inavyosimamia na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Ziara hiyo imefanyika katika Jiji la Dodoma, ambapo madiwani pamoja na wataalamu wa Halmashauri ya Buchosa wamepata fursa ya kujifunza mifumo na mbinu mbalimbali zinazotumiwa katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele katika ziara hiyo ni namna ya kuhakikisha mapato yanayostahili kukusanywa yanafika serikalini kwa kiwango cha juu, pamoja na kuweka mikakati ya kudhibiti mianya inayoweza kusababisha upotevu wa mapato.

Aidha, ujumbe wa Halmashauri ya Buchosa ulilenga kujifunza kutoka Dodoma namna wanavyowadhibiti wakwepa kodi na kuhakikisha wafanyabiashara pamoja na vyanzo mbalimbali vya mapato vinazingatiwa katika mfumo wa ukusanyaji.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Shigongo amewataka madiwani na wataalamu hao kutumia kikamilifu elimu na uzoefu walioupata jijini Dodoma ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ndani ya Halmashauri ya Buchosa.
Pia amesisitiza umuhimu wa kubaini na kudhibiti mianya inayosababisha mapato kupotea, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza uwezo wa Halmashauri kutoa huduma bora kwa wananchi.

Ziara hiyo, iliyoandaliwa kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za ukusanyaji wa mapato, imeonekana kuwa na manufaa kwa Halmashauri ya Buchosa.
Madiwani na wataalamu walioshiriki ziara hiyo wameahidi kutumia maarifa waliyoyapata kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kuongeza nguvu katika kudhibiti upotevu wa mapato.

Hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Buchosa kuongeza mapato yake na kuhakikisha rasilimali zinazokusanywa zinatumika ipasavyo kwa ajili ya maendeleo na huduma kwa wananchi.


