×

Mtanzania Neema Kengere Arejeshwa Tanzania Leo Kutoka Oman – Video

Mtanzania Neema Anthony Kengere, aliyekuwa amelazwa katika Wodi ya Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali ya Sohar nchini Oman, anatarajiwa kurejeshwa Tanzania leo, Septemba 9, 2026, kwa ajili ya kuendelea na matibabu.

Neema alipata matatizo ya kiafya akiwa nchini Oman, alikokwenda kufanya kazi. Hali yake ilizidi kuwa mbaya hadi kulazwa katika ICU akiwa hajitambui.

Jitihada za kuhakikisha Neema anarudishwa nchini zimefanywa kwa ushirikiano wa Ubalozi wa Tanzania nchini Oman, huku mtangazaji wa Kipindi cha Mapito, @zali_mapito, akisafiri hadi Oman kujionea hali ya Mtanzania huyo na kufuatilia hatua za kurejeshwa kwake nyumbani.

Safari hiyo imewezesha kukamilika kwa taratibu muhimu za kumsafirisha Neema kurejea Tanzania, kama ilivyokuwa ombi la familia yake.

Baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Neema atapelekwa moja kwa moja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kuendelea na matibabu.

Hospitali ya Taifa Muhimbili tayari imethibitisha kuwa imeandaa taratibu zote muhimu za kumpokea mgonjwa huyo. Gari la wagonjwa, daktari pamoja na nesi watakuwa wakimsubiri uwanjani ili kumpokea na kumpeleka hospitalini kwa haraka kwa ajili ya kupata huduma zaidi.

Taarifa zaidi kuhusu hali ya Neema na hatua zinazofuata zitakujia kupitia Global TV.

Stori na  ZALI MAPITO, GPL

Leave a Comment