
Klabu ya soka ya Young Africans (Yanga SC) imeanza utekelezaji wa mpango wake wa kuwekeza katika miundombinu ya kibiashara baada ya kubomoa rasmi jengo lake la zamani lililopo katika makutano ya Mtaa wa Mafia na Nyamwezi, Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Jengo hilo linatarajiwa kujengwa upya na kuwa jengo la kisasa la ghorofa 12, mradi unaolenga kuongeza vyanzo vya mapato ya klabu na kuimarisha uwezo wake wa kifedha kwa muda mrefu.
Hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa Yanga, chini ya Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said, kutangaza zabuni ya wazi kwa makampuni makubwa ya ujenzi yenye sifa na uzoefu, ili kupata kampuni itakayoshirikiana na klabu katika utekelezaji wa mradi huo.
Uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Yanga wa kupanua shughuli zake nje ya uwanja wa soka, kwa kutumia mali na miundombinu kama chanzo cha mapato ya kibiashara.
Uwanja wa Jangwani nao wajengwa
Mbali na mradi wa Kariakoo, Yanga pia inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 20,000 katika eneo la Jangwani, Dar es Salaam.

Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na GSM Group, ambaye ni mmoja wa washirika wakuu wa klabu hiyo katika uwekezaji na maendeleo ya miundombinu.
Bajeti ya Yanga yafikia Sh bilioni 36.01
Katika Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki, uongozi wa Yanga uliwasilisha mchanganuo wa kifedha wa klabu, ambapo wanachama waliidhinisha bajeti ya Sh bilioni 36.01 kwa matumizi ya klabu.
Bajeti hiyo imeongezeka kwa takribani Sh bilioni 3, kutoka Sh bilioni 33 zilizopangwa msimu uliopita, hali inayoonyesha kuongezeka kwa shughuli na mahitaji ya kifedha ya klabu.
Kwa ujumla, hatua za Yanga katika ujenzi wa jengo la Kariakoo na uwanja wa Jangwani zinaashiria mkakati wa klabu kujenga mali za kudumu na vyanzo endelevu vya mapato, sambamba na mafanikio yake ndani ya uwanja.
Na Peter Jinanai