
Kilimanjaro, Septemba 10, 2026 – Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania imezindua minara miwili mipya ya 4G mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni mwendelezo wa uwekezaji wake katika kupanua na kuboresha huduma za mawasiliano nchini.
Minara hiyo ambayo ipo katika wilaya ya Moshi Mjini na Mwanga inatarajiwa kuongeza uwezo na ubora wa mtandao, hususan huduma za intaneti, kwa wakazi, wafanyabiashara na taasisi katika maeneo hayo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Yas – Kanda ya Kaskazini, Robert Sanyagi, alisema uwekezaji huo unatokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za mawasiliano na matumizi ya huduma za kidijitali.

“Leo Watanzania wanahitaji zaidi ya huduma za kupiga simu. Wanahitaji intaneti yenye kasi na uhakika kwa ajili ya biashara, elimu, huduma za kifedha na shughuli nyingine za kila siku. Ndiyo maana tunaendelea kuwekeza katika teknolojia za 4G na 5G ili kuwafikia wananchi wengi zaidi,” alisema Sanyagi.
Alisema Yas itaendelea kupanua mtandao wake katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo maeneo ya mijini na pembezoni, ili wananchi wanufaike na fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Akizindua mnara huo, mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Moshi ambaye ni Afisa Tarafa wa Moshi Mashariki, Bi. Khalima Idrisa, amesema mnara huo utaimarisha mawasiliano na kusaidia juhudi za Serikali katika kuboresha huduma hizo kwa wananchi.
Kwa upande wake, mkazi wa Kilimanjaro, Bi. Mwanaisha Juma, aliishukuru Yas na kusema kuwa kuimarika kwa huduma za mawasiliano kutapunguza changamoto ambazo wananchi walikuwa wakikumbana nazo hapo awali.

“Zamani tulikuwa tunapata changamoto kubwa sana za kimawasiliano, hasa kwenye huduma za kutuma na kupokea fedha. Wakati mwingine fedha zilikuwa zinachelewa kufika.
Lakini sasa hivi hali imebadilika; huduma nyingi zinapatikana kwa urahisi kupitia mtandao. Tunaamini maboresho haya yataturahisishia zaidi maisha na shughuli zetu za kila siku,” alisema Bi.Mwanaisha.
Yas Tanzania imesema uzinduzi wa minara hiyo ni sehemu ya uwekezaji unaoendelea katika Kanda ya Kaskazini na maeneo mengine nchini, kwa lengo la kuwafikishia Watanzania huduma za mawasiliano zenye kasi na uhakika.