
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, amekumbwa na tukio la taharuki wakati akisafiri kutoka Moldova kuelekea Oslo, Norway, baada ya ndege aliyokuwa akisafiria kuripotiwa kuwa karibu kugongwa na drone.
Tukio hilo lilitokea wakati ndege ya Zelenskyy ikiwa inajiandaa kuondoka Moldova, ambako mamlaka ililazimika kufunga kwa muda anga ya nchi hiyo baada ya drone kuingia katika anga yake. Hatua hiyo ilisababisha safari kadhaa za ndege kuchelewa, ikiwemo ndege iliyokuwa imembeba Rais Zelenskyy.

Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Store, alithibitisha tukio hilo na kusema ndege ya Zelenskyy ilikuwa karibu kugongwa na drone wakati ikijiandaa kuruka kutoka Moldova. Hata hivyo, Store hakutoa maelezo kuhusu umbali ambao drone hiyo ilikuwa kutoka kwenye ndege au chanzo cha taarifa hizo.
Kwa upande mwingine, mamlaka za Moldova zilisema droni hiyo iliingia katika anga yao na baadaye ikaanguka katika eneo la Riscani, huku vipande vilivyopatikana vikionyesha sifa zinazofanana na drone aina ya Geran inayotumiwa na Urusi. Hakukuwa na taarifa za majeruhi kutokana na kuanguka kwa drone hiyo.

Zelenskyy alikuwa akielekea Oslo kuhudhuria mazishi ya Mfalme Harald V wa Norway, kabla ya kuendelea na ratiba zake za kidiplomasia. Tukio hilo limeongeza wasiwasi kuhusu usalama wa anga katika eneo hilo wakati vita vya Ukraine vikiendelea.