×

Wasusi Watakiwa Kutumia Programu ya Darling Hair Kujitanua Kibiashara

Dar es Salaam. Wasusi nchini wametakiwa kutumia kikamilifu programu ya Loyalty ya kampuni ya Darling Hair ili kujiongezea mitaji na kukuza biashara zao kupitia zawadi wanazopata kwa kukusanya pointi.

Wito huo umetolewa katika hafla ya kuadhimisha miaka miwili tangu kuanzishwa kwa programu hiyo, iliyofanyika katika ukumbi wa Sinza Deluxe, Dar es Salaam, ambapo wasusi kutoka Tabata, Mbezi, Kimara na maeneo ya jirani walishiriki katika shughuli mbalimbali za burudani, michezo, chakula pamoja na kujishindia zawadi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Salma Hamadi kutoka Tabata alisema programu hiyo imekuwa na mchango mkubwa kwa wasusi, huku baadhi yao wakitumia zawadi wanazopata kuongeza mitaji na wengine kuweza kufungua saluni zao.

“Programu hii sasa ina miaka miwili na tayari tumeona makubwa ambayo imetufanyia kama wasusi. Baadhi yetu tumeongeza mitaji na wengine ambao walianza kama wasusi wa kuajiriwa sasa wana saluni zao baada ya kujishindia vifaa mbalimbali vya saluni,” alisema Hamadi.

Alisema programu hiyo imewapa wasusi fursa ya kukutana, kubadilishana uzoefu na kupata motisha ya kuendeleza biashara zao, huku akiipongeza Darling Hair kwa kuwa karibu na kundi hilo.

Kwa upande wake, Doreen Didas wa Mbezi Mwisho aliwataka wasusi kuongeza juhudi katika kukusanya lebo ili kuongeza nafasi ya kushinda zawadi kubwa zinazoweza kuwasaidia kupanua biashara zao.

“Unaweza kuwa msusi mdogo tu lakini Darling Hair wakakusaidia kukua polepole kupitia programu hii ya Loyalty,” alisema.

Msusi mwingine, Shantel Mushi wa Tabata Mawenzi, alisema programu hiyo ina manufaa makubwa kwa wasusi na kuwataka wale ambao bado hawajajiunga kufanya hivyo ili nao wanufaike.

“Natamani wasusi wote waijue programu hii ya Loyalty kwani Darling wamekuja na kitu cha kipekee chenye faida kubwa mno kwa wateja, yaani sisi wasusi. Ambao hamjajiunga mmechelewa sana, ila bado mna nafasi ya kujiunga na kunufaika kama sisi,” alisema.

Naye Angel Ngita wa Tabata alisema wasusi wanapaswa kuwa na subira na kuweka malengo ya muda mrefu badala ya kukimbilia kutumia zawadi wanazopata.

“Mimi leo nimeshinda lakini sichukui zawadi hii, naendelea kukusanya pointi ziwe nyingi ili nipate kitu kikubwa zaidi. Nimeingia kwenye programu hii na malengo ili niweze kujiendeleza,” alisema Ngita.

Christina Mbando wa Tabata pia aliishukuru Darling Hair kwa kuendelea kuwa karibu na wasusi na kuwafuatilia katika hatua mbalimbali za ukuaji wa biashara zao.

“Hakuna kampuni inayofanya kama Darling Hair. Tunawaomba wasiachie programu hii ili sisi wasusi tuendelee kunufaika zaidi,” alisema.

Programu kupelekwa mikoani

Mwakilishi wa Darling Hair, Daniel Kisusange, alisema kampuni hiyo imepanga kupeleka programu hiyo katika mikoa mbalimbali ili kuhakikisha wasusi wengi zaidi nchini wanapata fursa ya kunufaika.

“Tunawaomba mjiandae, tunakuja huko maana kampeni hii ni ya nchi nzima na lengo ni kuendelea kuwafikia wasusi wengi zaidi,” alisema Kisusange.

Alifafanua kuwa programu hiyo ilianza ikiwa na wasusi takribani 5,000 katika mwaka wake wa kwanza, lakini idadi hiyo imeongezeka na kufikia zaidi ya 10,000 wanaonufaika na programu hiyo.

Kwa mujibu wa Kisusange, programu ya Loyalty inalenga kuwawezesha wasusi wadogo kujenga mitaji na kukuza biashara zao kupitia mfumo wa pointi na zawadi mbalimbali, zikiwemo vifaa vinavyoweza kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku.

Aliwahimiza wasusi kuendelea kutumia programu hiyo kwa malengo ya kujitanua zaidi, akisisitiza kuwa ni mpango wa muda mrefu wa kampuni hiyo unaolenga kuendelea kuwawezesha wasusi nchini.

Leave a Comment