×

Heche Aulizwa Uraia wa Mke na Watoto wa Lissu, Asema Hajui

Familia ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, imeibua mjadala mwingine katika kesi hiyo ya uhaini inayokabili baada ya wakili Nassoro Katuga kumuuliza shahidi John Heche kuhusu uraia wa baadhi ya wanafamilia wa Mwenyekiti huyo, huku Heche akisema hajui kama watoto na mke wa Lissu si raia wa Tanzania.
Katika mahojiano ya kuhojiwa na Nassoro Katuga, Heche alikiri kuwa hajui iwapo watoto wa Lissu, ambaye amekuwa akimtaja kama mzalendo, ni raia wa Tanzania, licha ya kukubali kuwa Tanzania haina uraia wa nchi mbili.
Katuga alimuuliza Heche kama anafahamu kuwa Mwenyekiti anayemtaja kuwa mzalendo ana watoto ambao si raia wa Tanzania, ambapo Heche alijibu kuwa jambo hilo halijui. Alipoulizwa kuhusu mke wa Mwenyekiti huyo, Heche pia alisema hajui kuhusu uraia wake, akisisitiza kuwa anachojua ni kwamba ni Mkurya.

Katika sehemu nyingine ya ushahidi wake, Heche alieleza kuhusu kifo cha mdogo wake, Suguta Heche, akisema yeye mwenyewe hakuwapo wakati mdogo wake alipokuwa akiteswa na kuchomwa kwa singe, bali taarifa hizo alizipata kutoka kwa RPC.
Katuga alitaka kufahamu iwapo Heche alishuhudia tukio hilo moja kwa moja, lakini Heche alisisitiza kuwa taarifa hizo zilitolewa na RPC. Vilevile, alipoulizwa sehemu ya mwili ambayo Suguta alichomwa kwa singe, Heche alisema hakueleza Mahakamani.

Heche pia alikiri kuwa hakuwapo eneo ambalo polisi walidaiwa kutaka kumtupa mdogo wake, akisema taarifa hiyo aliipata kutoka kwa RPC. Aidha, alikiri kuwa mtu anayemtuhumu kwa kumuua mdogo wake hakumtaja jina Mahakamani.
Katika mahojiano hayo, Katuga alitaka kujua kama mtu huyo aliwahi kumweleza Heche kwamba alimuua Suguta kwa lengo la kumtisha ili asiendelee na shughuli zake za kisiasa.

Heche alijibu kuwa mtuhumiwa huyo hakuwahi kumweleza hivyo. Hata hivyo, alirejea kauli ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli, kwamba mpaka mwaka 2020 upinzani ungekuwa umeisha.
Alipoulizwa kama sababu ya mauaji hayo ilikuwa ni kumkomoa yeye kisiasa, Heche alisema, “Mimi najua ni mimi,” huku akikiri kuwa hakuwahi kuambiwa moja kwa moja na mtuhumiwa kwamba alimuua mdogo wake kwa sababu hiyo.

Leave a Comment