×

Mauaji ya Kijana Moshi Yazua Vurugu, Gari Lachomwa Moto, Polisi Waonya Wananchi

Moshi, Kilimanjaro — Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limeanzisha uchunguzi wa tukio la mauaji ya kijana Steven Karakira Kaaya (24), mkazi wa Mtaa wa Boma Mbuzi, Wilaya ya Moshi, ambaye alifariki baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa kitu cha plastiki.

Tukio hilo lilitokea Septemba 13, 2026, majira ya saa 11:00 jioni, katika eneo la Mtaa wa Spencorn, Kata ya Bomambuzi, Wilaya ya Moshi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, wakati wa tukio hilo kijana huyo alishambuliwa katika sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia kitu butu na watu ambao majina yao hayajajulikana. Alidaiwa kuhusishwa na tabia ya kuchunguza vitu vya watu mbalimbali kwa nia ya kuiba.

Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa mmoja kwa mahojiano zaidi huku uchunguzi ukiendelea ili kubaini na kuwakamata watu wengine waliohusika na tukio hilo.

Aidha, baada ya tukio la mauaji kutokea, baadhi ya wananchi walijichukulia sheria mkononi kwa kufanya vurugu na kusababisha uharibifu wa mali, ikiwemo kuchoma moto gari aina ya Mitsubishi Canta, yenye namba za usajili T.119 ATV, linalodaiwa kuwa la mmoja wa watu waliotuhumiwa kuhusika na tukio hilo.

Vilevile, baadhi ya mali zilizokuwa ndani ya chumba cha duka linalomilikiwa na Thelesia Omary Nyambuleki Mwikoma ziliripotiwa kuharibiwa katika vurugu hizo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Jeshi hilo pia limeeleza kuwa chanzo na mazingira halisi ya tukio bado vinaendelea kuchunguzwa kwa kushirikiana na taasisi na mamlaka nyingine. Hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na mauaji, vurugu na uharibifu wa mali.

Leave a Comment