
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limethibitisha kifo cha mwanaume mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 35, baada ya kupigwa risasi alipokuwa akijaribu kutekeleza uhalifu katika Benki ya CRDB, Tawi la Rock City Mall, Wilaya ya Ilemela.
Tukio hilo lilitokea Septemba 13, 2026 majira ya saa 7:58 mchana, ambapo mwanaume huyo alifika benki akiwa amevalia kofia, shati la mikono mirefu, suruali ya jeans na viatu vya wazi.
Awali, alimuomba mhudumu fedha akidai anahitaji fedha za kula. Baada ya kukataliwa, aliingia katika eneo la kaunta na kuelekea kwenye sehemu ya kuhifadhi fedha, hali iliyosababisha taharuki kwa wafanyakazi na wateja.
Askari waliokuwa wakilinda benki walifika na kumtaka ajisalimishe, lakini alikaidi amri na kuanza kukabiliana na askari, akijaribu pia kuwanyang’anya silaha.
Katika hatua hiyo, askari walimpiga risasi kwenye mguu wa kulia ili kumdhibiti.
Alikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Sekou-Toure kwa matibabu, lakini alifariki akiwa hospitalini.
Mwili wake umehifadhiwa hospitalini kwa ajili ya utambuzi na hatua nyingine za uchunguzi. Polisi pia walimkuta na simu aina ya Samsung pamoja na Shilingi 500.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

