×

Wafanyabiashara 150 Mwanza Wapatiwa Mafunzo ya Kuimarisha Biashara

Zaidi ya wafanyabiashara 150 jijini Mwanza wamepatiwa mafunzo ya uendeshaji wa biashara, usimamizi wa fedha na matumizi ya teknolojia, kupitia Mpango wa Maendeleo ya Wafanyabiashara wa Rejareja (GRIT).

Mafunzo hayo, yanayotekelezwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa ushirikiano na Vodacom Tanzania Plc, yamewakutanisha wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kuendesha biashara zao kwa ufanisi na kukuza faida.

Washiriki wamefundishwa namna ya kusimamia fedha, kupanga matumizi, kudhibiti bidhaa, kufuatilia mauzo na gharama, pamoja na kufanya maamuzi yanayoweza kusaidia biashara zao kukua kwa muda mrefu.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, alisema mpango wa GRIT ni sehemu ya juhudi za kampuni hiyo kuwawezesha wafanyabiashara wanaofanya kazi nayo kwa kuwapatia maarifa na ujuzi unaoweza kuwasaidia kusimamia biashara zao kwa ufanisi zaidi.

Kilpin alisema uwezo wa kusimamia fedha, bidhaa na shughuli za kila siku ni muhimu katika kuiweka biashara katika nafasi nzuri ya kukua na kuchangia maendeleo ya jamii.

Miongoni mwa wakufunzi alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Patrokil Kanje, aliyewafundisha washiriki namna ya kuendesha biashara kwa ufanisi, kudhibiti gharama na kutambua maeneo yanayoweza kuongeza faida.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Dkt. Kanje aliwasisitiza wafanyabiashara kuwa na uelewa wa kina kuhusu biashara zao, hususan katika kufuatilia mauzo, gharama na faida.

Alisema mfanyabiashara hapaswi kuangalia kiasi cha fedha anachopata kutokana na mauzo pekee, bali pia anatakiwa kufahamu gharama anazotumia na faida halisi inayobaki, kwa kuwa taarifa hizo ni muhimu katika kufanya maamuzi sahihi na kupanga ukuaji wa biashara.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Masoko na Uwezeshaji wa Vodacom Tanzania Plc, Joseph Sayi, aliwahimiza wafanyabiashara kutumia suluhisho za kidijitali katika shughuli zao za kila siku.

Sayi alisema matumizi sahihi ya teknolojia yanaweza kurahisisha miamala, kusaidia usimamizi wa fedha, kuimarisha mawasiliano na wateja pamoja na kuwezesha wafanyabiashara kupata huduma mbalimbali kwa urahisi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa miaka miwili kati ya TBL na Vodacom Tanzania, unaolenga kuwafikia zaidi ya wafanyabiashara 24,000 wa TBL nchini.

Kupitia mpango wa GRIT, wafanyabiashara wanatarajiwa kupata ujuzi katika maeneo mbalimbali, yakiwemo usimamizi wa mtaji na mtiririko wa fedha, udhibiti wa bidhaa, huduma kwa wateja, ukuaji wa biashara pamoja na matumizi ya teknolojia na suluhisho za kidijitali.

Kwa wafanyabiashara walioshiriki mafunzo hayo jijini Mwanza, mpango huo unatoa fursa ya kuangalia biashara zao kwa mtazamo mpana zaidi, kwa kuzingatia si mauzo ya siku hiyo pekee, bali pia namna ya kujenga biashara inayoweza kusimamiwa kwa ufanisi, kukabiliana na changamoto na kukua kwa muda mrefu.

Mpango huo unatarajiwa kuendelea kuwafikia wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali nchini, ukiweka mkazo katika kuwapatia maarifa na zana za kuwasaidia kuendesha biashara kwa ufanisi zaidi katika mazingira ya biashara yanayobadilika.

Leave a Comment