
Mshtakiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amemaliza kumuuliza maswali ya re-examination shahidi wake, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche, katika kesi inayosikilizwa mbele ya Jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu, likiongozwa na Jaji Dustan Ndunguru.
Baada ya kumaliza kumuuliza Heche maswali ya re-examination, Lissu aliliomba Jopo la Majaji maelekezo kuhusu mashahidi ambao Mahakama ilitoa summons kwa ajili yao.

“Waheshimiwa Majaji, niliomba summons kwa ajili ya mashahidi, kwa hiyo nataka kujua majibu kuwa mashahidi hao wako wapi na tunakwendaje mbele,” alisema Lissu.
Lissu alieleza pia kuwa anahitaji kukutana na mashahidi hao kabla hawajafika mahakamani ili kuwaandaa kwa ajili ya kutoa ushahidi.
Alisema hawezi kuwaweka mashahidi kizimbani bila kwanza kukutana nao na kuwaelekeza namna ya kuendesha ushahidi wao.
Kwa mujibu wa Lissu, Mahakama ndiyo eneo pekee analoweza kukutana na mashahidi hao kwa kuwa hana sehemu nyingine ya kuwaandalia, huku akisema hawezi kwenda maofisini kwao au gerezani.

Jaji Ndunguru alisema Mahakama ilitarajia upande wa Lissu kutoa taarifa iwapo ana shahidi au hana, kwa kuwa summons tayari zilitolewa na Mahakama.
Jaji alisema Mahakama ingepumzika ili Msajili awasilishe taarifa kuhusu utekelezaji wa summons hizo.
Baada ya mapumziko, Lissu alirejea mahakamani na kueleza kuwa alikuwa amekutana na Msajili wa Mahakama ambaye alimpatia taarifa kuhusu summons za mashahidi.
Kwa mujibu wa Lissu, Msajili alimweleza kuwa mashahidi wote walipelekewa summons Dodoma, ingawa nakala za summons hizo hazikuweza kuhifadhiwa baada ya kubainika kuwa baadhi ya mashahidi walikuwa nje ya nchi.

Lissu alisema mmoja wa mashahidi hao, ambaye ni Kamishna wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi katika Jeshi la Polisi (DCI), alitarajiwa kurejea nchini siku hiyo.
Alisema Msajili alimwahidi kuwa siku ya Ijumaa Kamishna huyo atakuwepo Mahakamani kwa ajili ya kutekeleza wito uliotolewa na Mahakama.
Lissu alieleza kuwa mashahidi wengine wawili waliotajwa ni Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob Mkunda, na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camillius Wambura, ambao wakati huo haikufahamika ni lini wangerejea nchini.

Kutokana na hali hiyo, Lissu alipendekeza kesi hiyo iahirishwe hadi Ijumaa saa 8:30 mchana, ili muda wa asubuhi autumie kukutana na kushauriana na shahidi anayetarajiwa kufika, pamoja na kuchukua maelezo yake.
Alisema endapo mashahidi hao hawatakuja kabisa, suala hilo litakuwa mikononi mwa Mahakama kwa kuwa ni Mahakama iliyotoa summons hizo.
Aidha, Lissu alieleza kuwa anafahamu ratiba ya shauri hilo ilivyo na kwamba yeye pia anatamani shauri hilo lifikie hatua ya final submissions ili Mahakama ipate muda wa kutafakari na kutoa uamuzi.

Alisema iwapo mashahidi watafuata wito wa Mahakama, anaamini ushahidi wao hautachukua muda mrefu.
Upande wa mashtaka, kupitia Wakili Nassor Katuga, ulisema hauna pingamizi kuhusu kuahirishwa kwa kesi hiyo.
“Hata hivyo, tunaomba Mahakama hii imsisitize mshtakiwa mashahidi wake wafike kwa wakati,” alisema Katuga.
Kauli hiyo ilisababisha hali vicheko mahakamani, kabla ya Jaji Ndunguru kusisitiza kuwa mashahidi hao si “mashahidi wake” kwa maana ya kwamba ni jukumu la Mahakama kuhakikisha summons zinazingatiwa, huku akimkumbusha Lissu kuwa yeye ndiye anayetarajiwa kuwaleta mashahidi hao mahakamani.
Hatimaye, Jaji Ndunguru alitangaza kuwa shauri hilo limeahirishwa hadi Ijumaa tarehe 18, ambapo shahidi anayetarajiwa kufika mahakamani anatarajiwa kuendelea na hatua inayofuata ya ushahidi.
Katika hatua hiyo, Ramadhan Kingai anatarajiwa kufika Mahakamani Ijumaa kwa ajili ya kutoa ushahidi, ikiwa ni sehemu ya mwenendo wa shauri hilo.