×

Pablo Franco Atoa Somo Morocco, Atwaa Tuzo Ya Kocha Bora

Aliyekuwa Kocha Mkuu wa klabu ya Simba SC ya Tanzania na AmaZulu ya Afrika Kusini, raia wa Hispania, Pablo Franco Martín, ametangazwa rasmi kuwa Kocha Bora wa Mwaka wa Ligi Kuu ya Morocco, Botola Pro 1, kwa msimu wa 2025/26.

Tuzo hiyo imekuja kufuatia mafanikio makubwa ya kihistoria aliyoyapata kocha huyo baada ya kuiongoza klabu ya Maghreb Fès (MAS Fès) kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Morocco, taji ambalo klabu hiyo ilikuwa imelilikosa kwa miaka 46.

Katika kinyang’anyiro hicho, Pablo amewashinda wapinzani wake wa karibu, Alexander Santos, aliyekuwa akiifundisha AS FAR Rabat, pamoja na Mouine Chaabani wa RS Berkane, kufuatia kura zilizopigwa na wadau pamoja na jopo la wataalamu wa soka nchini Morocco.

Chini ya ukufunzi wa Pablo Franco, Maghreb Fès ilimaliza msimu ikiwa kileleni mwa msimamo baada ya kucheza michezo 30, ambapo ilikusanya alama 59. Katika michezo hiyo, timu hiyo ilipata ushindi katika mechi 16, kutoka sare mara 11 na kupoteza michezo mitatu pekee.

Safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ilifunga mabao 40, huku safu ya ulinzi ikiruhusu mabao 17 pekee.

Ubingwa huo ulikamilika kwa ushindani mkali, kwani Maghreb Fès ilitwaa taji hilo kwa tofauti ya alama mbili tu mbele ya washindi wa pili, RS Berkane, na alama tatu mbele ya miamba ya Raja Casablanca.

Mafanikio haya yanaendelea kupandisha wasifu wa kocha huyo mwenye leseni ya UEFA Pro, ambaye amewahi pia kuhudumu kama kocha msaidizi wa Real Madrid nchini Hispania.

Ushindi huu unaandika ukurasa mpya wa mafanikio katika taaluma yake barani Afrika, baada ya vipindi vyake vya nyuma katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

Stori na Peter Jinanai | GPL

Leave a Comment