Dar es Salaam, Tanzania — Septemba 17, 2026: Serengeti Lite, kwa kushirikiana na KUNTA Africa, imetangaza rasmi kurejea kwa Nyota Bigi msimu wa pili, mpango unaolenga kusaka na kukuza vipaji vipya vya ubunifu nchini Tanzania.
Usaili wa msimu huu utafanyika katika mikoa minne, ambapo safari ya kusaka vipaji itaanzia Dar es Salaam Oktoba 3, ikifuatiwa na Mwanza Oktoba 10, Arusha Oktoba 17, na kuhitimishwa Dodoma Oktoba 24, 2026.
Nyota Bigi msimu wa pili unalenga kuwapa nafasi waimbaji, wacheza muziki, waigizaji, wachekeshaji, wabunifu wa mitindo pamoja na watu wenye vipaji mbalimbali vya ubunifu ambavyo bado havijapata nafasi ya kutambulika kwa hadhira kubwa.

Mpango huo ni sehemu ya kampeni ya Serengeti Lite inayojulikana kama “Lite Your Imagination”, inayolenga kuwahamasisha vijana kutambua uwezo wao wa ubunifu, kujiamini na kutumia vipaji vyao kama fursa ya kujenga maisha na taaluma.
Akizungumza katika uzinduzi wa msimu wa pili jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masoko na Ubunifu wa Serengeti Breweries, Henry Esiaba, alisema Nyota Bigi inalenga kutoa jukwaa kwa vijana wenye vipaji kutoka maeneo mbalimbali nchini.
“Tuna vipaji vingi katika kila kona ya nchi hii. Ila kinachokosekana wakati mwingine ni nafasi ya kuonekana. Nyota Bigi ipo kwa ajili ya kuwapa vijana wa Tanzania jukwaa hilo,” alisema Esiaba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Bia wa Serengeti Breweries, Rhona Namanya, alisema msimu wa pili umeongezwa wigo kwa kufikisha mchakato wa kusaka vipaji katika miji zaidi ikilinganishwa na msimu uliopita uliofanyika Dar es Salaam pekee.
Namanya amesema hatua hiyo inalenga kuongeza nafasi kwa vijana wenye vipaji kutoka mikoa mbalimbali nchini kushiriki na kupata fursa ya kutambulika.
Kwa mujibu wa waandaaji, usajili tayari umefunguliwa kupitia msimbo wa QR wa Nyota Bigi, tovuti, WhatsApp au simu. Waombaji wanatakiwa kuwa na umri wa kati ya miaka 18 hadi 35, kitambulisho halali na video fupi inayoonyesha kipaji chao.
Usaili utafanyika ana kwa ana pamoja na mtandaoni, hatua inayolenga kuwawezesha washiriki kutoka maeneo mbalimbali kushiriki katika mchakato huo.
Mbali na mashindano, washiriki watakaofanya vizuri watapata fursa ya kuunganishwa na wadau mbalimbali wa sekta ya ubunifu, ikiwemo mitandao ya kijamii, uanamitindo, burudani, usimamizi wa vipaji na studio za kurekodi.
Kupitia Nyota Bigi, Serengeti Lite na KUNTA Africa zinalenga kuendelea kutoa jukwaa kwa vijana kuonyesha uwezo wao na kuendeleza vipaji vyao katika sekta ya ubunifu nchini Tanzania.
