
DAR ES SALAAM — Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na halmashauri zake kuhakikisha hali ya Dampo la Pugu inaboreshwa na kero za wananchi wanaoishi maeneo ya jirani zinapatiwa ufumbuzi.

Ndejembi ametoa agizo hilo leo, Septemba 18, 2026, alipofanya ziara katika Dampo la Pugu linalotumika kukusanya taka za Mkoa wa Dar es Salaam, kwa lengo la kujionea hali halisi ya eneo hilo na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi wanaoishi jirani na dampo hilo.

Makamu wa Rais ameelekeza maeneo ya makazi yanayozunguka Dampo la Pugu kupuliziwa dawa za kuua wadudu, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuwalinda wananchi dhidi ya wadudu na kupunguza hatari ya magonjwa, hususan wakati wa kipindi cha mvua.
Aidha, ameagiza kuandaliwa kwa mpango kazi wa pamoja utakaobainisha hatua za haraka na za muda mrefu za kukabiliana na changamoto za uendeshaji wa dampo hilo pamoja na kero zinazowakabili wananchi wanaoishi maeneo yanayolizunguka.

Akiwa katika eneo hilo, Mhe. Ndejembi ameonesha kutoridhishwa na kutofautiana kwa takwimu zinazotolewa kuhusu kiasi cha taka kinachokusanywa na kupelekwa Dampo la Pugu kila siku kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.
Kutokana na hali hiyo, amezitaka mamlaka zote zinazohusika kukaa pamoja, kuhakiki na kuweka takwimu sahihi zitakazotumika kama msingi wa kupanga na kutekeleza hatua madhubuti za kuboresha usimamizi wa taka jijini.

“Hatuwezi kutatua changamoto za eneo hili bila kuwa na taarifa na takwimu sahihi. Hawa wananchi mnaowaona wamechoka na stori; wanataka kuona kazi,” amesisitiza Makamu wa Rais.
Amesema wananchi wanatarajia kuona matokeo ya moja kwa moja kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali, hivyo amewataka viongozi na taasisi husika kuharakisha utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu kutatua kero za wananchi.
Ndejembi amesisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Serikali inayosikiliza wananchi na inayojali maslahi yao, akiahidi kuwa changamoto zinazowakabili zitaendelea kushughulikiwa kwa wakati.





