×

SGR na JKCI Waanzisha Ushirikiano wa Kutoa Huduma Za Afya Kwa Abiria

Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) zimeingia katika ushirikiano wa kimkakati wa kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, hatua itakayoanza kwa utoaji wa huduma za uchunguzi na vipimo vya afya ya moyo bila malipo kwa abiria wanaosafiri kwa treni ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) kati ya Dar es Salaam na Dodoma.

Kupitia ushirikiano huo, huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza zitatolewa ndani ya treni za SGR kuanzia Septemba 21 hadi 27, 2026, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Afya ya Moyo kuelekea Siku ya Moyo Duniani inayoadhimishwa Septemba 29 kila mwaka.

Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 18, 2026, katika Stesheni ya SGR jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa JKCI, Dkt. Peter Kissenge, alisema wataalamu na mabingwa wa afya watasafiri ndani ya treni hizo kutoa huduma za uchunguzi, ushauri na elimu ya afya kwa abiria watakaohitaji huduma hizo.

Alisema vipimo vitakavyotolewa ni pamoja na Echo, ECG, vipimo vya sukari na mafuta kwenye damu, ambavyo kwa kawaida vina gharama kubwa vinapotolewa hospitalini.

“Vipimo hivi vyote vinaweza kugharimu zaidi ya shilingi 500,000 vinapofanyika hospitalini, lakini katika kipindi hiki cha Wiki ya Afya ya Moyo vitatolewa bila malipo kwa abiria wote watakaosafiri kwa SGR,” alisema Dkt. Kissenge.

Aliongeza kuwa mpango huo unalenga kuhamasisha wananchi kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini mapema magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza ambayo yanaendelea kuongezeka nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Masanja Machibya, alisema ushirikiano huo unaashiria mwanzo wa hatua mpya ya kuunganisha huduma za usafiri na afya kwa manufaa ya wananchi.

Alisema TRC inaendelea na maandalizi ya mradi wa mabehewa maalumu ya matibabu yatakayokuwa na vifaa vya kisasa pamoja na vitanda kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa mahututi na wanaopewa rufaa kutoka mikoani kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa haraka na usalama zaidi.

“Mabehewa haya yatasaidia kupunguza muda wa usafirishaji wa wagonjwa kutoka mikoa mbalimbali, hususan Dodoma na Morogoro, na kuwafikisha kwa haraka zaidi katika vituo vya matibabu vya rufaa ikilinganishwa na usafiri wa barabarani,” alisema Machibya.

Alibainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza ndani ya miezi sita ijayo, hatua inayotarajiwa kuimarisha huduma za afya na mfumo wa rufaa nchini.

Aidha, wananchi na abiria wote watakaosafiri kwa SGR katika kipindi hicho wamehimizwa kutumia fursa hiyo ya kupata uchunguzi wa afya ya moyo na ushauri wa kitaalamu bila gharama, ili kubaini mapema changamoto za kiafya na kuchukua hatua stahiki za matibabu.

Leave a Comment