×

Idris Sultan Kuiwakilisha Tanzania Kwenye Tuzo Kubwa Afrika Novemba 2026

MTANZANIA Idris Sultan amepewa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika moja ya majukwaa makubwa yanayotambua na kuenzi vijana wenye mafanikio barani Afrika.

Idris, ambaye ni mwigizaji, mchekeshaji na mtayarishaji, ametangazwa kuwa mmoja wa waandaji wa The Future Awards Africa (TFAA) 2026, hafla kubwa inayotarajiwa kufanyika mwezi Novemba 2026 katika Balmoral Events Centre, Lagos, Nigeria.

Idris atakuwa miongoni mwa waandaji watano kutoka nchi mbalimbali za Afrika, akiiwakilisha Tanzania katika jukwaa hilo pamoja na wawakilishi kutoka Nigeria, Kenya, Malawi na Botswana.

Waandaji wengine waliotangazwa ni mwigizaji wa Nigeria, Genoveva Umeh; mtangazaji wa Malawi, Priscilla Kayira; mtangazaji na mtayarishaji kutoka Botswana, Resego Motlhokathari; pamoja na mwanahabari na mwigizaji wa Kenya, Claudia Naisibwa.

Kwa mwaka huu, TFAA inaadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, huku waandaaji wakitumia mfumo wa kipekee wa kuwaleta pamoja waandaji watano kutoka mataifa matano tofauti ya Afrika kwenye jukwaa moja.

Kaulimbiu ya TFAA 2026 ni “Celebrating the Redefiners: Africa’s AI Generation,” inayolenga kuangazia kizazi kipya cha vijana wa Afrika wanaotumia teknolojia, ubunifu na mawazo mapya kubadilisha sekta mbalimbali.

Nafasi hiyo inampa Idris Sultan fursa ya kuendelea kuonekana katika jukwaa la kimataifa na kushiriki katika tukio linalolenga kutambua mchango na mafanikio ya vijana barani Afrika.

Stori na Razaku Ramadhan | GPL – TUDACO

Leave a Comment