
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inatarajiwa kuanza kampeni yake ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kwa mchezo dhidi ya Guinea-Bissau.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Septemba 18, 2026, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, amesema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Septemba 25, 2026 katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Baada ya mchezo huo, Taifa Stars inatarajiwa kusafiri Septemba 26 kuelekea Casablanca, Morocco, kwa ajili ya mchezo wa pili wa kampeni hiyo dhidi ya Madagascar.
Madagascar imechagua Morocco kuwa eneo la kuchezea kama mwenyeji wa mchezo huo, ambao unatarajiwa kufanyika Septemba 29, 2026.
Mbali na michezo hiyo ya kufuzu AFCON, Taifa Stars pia inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Ghana.
Mchezo huo wa kirafiki umepangwa kuchezwa Oktoba 4, 2026 jijini Casablanca, Morocco, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya timu hiyo kwa michezo yake ijayo.
Taifa Stars sasa inaelekeza nguvu katika maandalizi ya mchezo wa kwanza dhidi ya Guinea-Bissau, huku ikitarajiwa kutumia michezo hiyo kujenga msingi mzuri katika safari ya kuwania nafasi ya kushiriki AFCON 2027.
Stori Na Clever Alphonce | GPL -TUDACO