×

Waziri Katambi Atoa Ufafanuzi kuhusu Mfumo wa Alama za leseni

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Paschal Katambi Patrobass, amesema Serikali imeanza kufanya majaribio ya mfumo wa alama za leseni za udereva kwa lengo la kudhibiti makosa ya usalama barabarani na kupunguza ajali nchini.

Akizungumza kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa Septemba 19, 2026, Waziri Katambi amesema mfumo huo unatokana na Kanuni za Usalama Barabarani (Mfumo wa Alama za Leseni za Udereva) za mwaka 2014, ambazo zilirekebishwa mwaka 2025.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chini ya Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, Waziri mwenye mamlaka ya kutunga kanuni kuhusu masuala ya usalama barabarani anaweza kuweka mfumo wa kupunguza vifo na ajali zinazotokana na sababu mbalimbali, ikiwemo makosa yanayofanywa na madereva wa vyombo vya usafiri.

Serikali imeeleza kuwa imefanya kazi ya muda mrefu na imejiridhisha kuwa hakuna haja ya kuanza kutumia mfumo huo madhubuti wa kudhibiti usalama barabarani.

Aidha, Serikali imeeleza kuwa pamoja na miradi ya usalama barabarani inayoendelea, ikiwemo matumizi ya teknolojia za kamera za barabarani zenye uwezo wa kutumia akili unde (AI), imeanza majaribio ya mfumo wa alama za leseni za udereva.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa mfumo huo bado haujaanza kutumika rasmi, bali hatua ya sasa ni kufanya majaribio ili kubaini namna utakavyoweza kutumika kudhibiti madereva watakaokiuka Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani.

Serikali imeonya madereva kuwa leseni zao zikiingizwa kwenye mfumo huo, alama zitakazotolewa kutokana na makosa ya barabarani zinaweza kuathiri uhalali wa leseni zao iwapo wataendelea kukiuka sheria.

Waziri Katambi amesema baadhi ya alama zinazoweza kuhusishwa na makosa ya barabarani ni pamoja na makosa ya mwendokasi, kutofuata alama za barabarani, kuzidisha abiria, kutoa mikanda, kuendesha vyombo hatarishi na makosa mengine kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168.

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza ajali za barabarani zinazosababisha vifo na majeruhi, akieleza kuwa matumizi ya mifumo kama hiyo yamekuwa yakiongezeka katika nchi mbalimbali.

Ametolea mfano Rwanda, ambayo amesema imetumia mfumo huo na kuona kupungua kwa kiwango kikubwa cha ajali na vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.

Waziri Katambi pia amesisitiza kuwa Kanuni za Usalama Barabarani (Mfumo wa Alama za Leseni za Udereva) za mwaka 2014, zilizorekebishwa mwaka 2025, bado hazijaanza kutekelezwa rasmi.

Amesema sababu mojawapo ya kutocheleweshwa kwa utekelezaji wake ni kuwa wataalamu wa mifumo kutoka Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mapato wanaendelea kuunganisha mifumo hiyo ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Sababu nyingine, kwa mujibu wa Waziri, ni kwamba Serikali iko katika kipindi cha utoaji elimu kwa umma kuhusu kanuni hizo. Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani linaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya madereva wa vyombo vya moto pamoja na wananchi kwa ujumla kuhusu mfumo huo na umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Waziri amesema Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani linaendelea kufikisha elimu hiyo kwa makundi mbalimbali ya madereva kupitia mikutano ya uelimishaji, pamoja na vyombo vya habari kama redio na Runinga, katika vituo vya mabasi, maeneo ya maegesho ya malori, mikusanyiko ya watu na maeneo mengine.

Ameongeza kuwa elimu hiyo inalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu makosa yanayoweza kupewa alama na namna alama hizo zitakavyotumika.

Waziri Katambi amesisitiza kuwa mfumo huo bado haujaanza kutekelezwa rasmi, hivyo hakuna haja ya dereva ambaye leseni yake imeondolewa alama kutokana na kosa la barabarani kuwa na wasiwasi kwa sasa.

Amesema madereva watajulishwa rasmi pindi mfumo huo utakapoanza kutumika.

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Paschal Katambi Patrobass, Septemba 19, 2026, jijini Dar es Salaam.

Leave a Comment