Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa adhabu mbalimbali kwa klabu, viongozi na waamuzi kufuatia mwenendo wa michezo ya Ligi Kuu ya NBC na Championship, katika kikao chake kilichofanyika Septemba 18, 2026.
Katika Ligi Kuu ya NBC, Young Africans SC imetozwa faini ya Sh milioni 5 kwa kosa la mashabiki wake kuwarushia chupa benchi la ufundi la Geita Gold katika mchezo uliomalizika kwa Yanga kushinda 1-0.
Mbali na faini hiyo, Yanga imepewa onyo kali kwa kutofuata mtiririko wa matukio ya mchezo (Match Countdown), ambapo wachezaji watatu waliingia uwanjani kwa ajili ya kupasha misuli joto saa 12:00 jioni badala ya saa 12:10 jioni kama ilivyopangwa.
Aidha, Afisa Ulinzi na Usalama wa Yanga, Eddie Evance, amepelekwa Kamati ya Maadili ya TFF kwa kosa la kukaidi maamuzi ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi. Evance alionekana uwanjani wakati wa mchezo huo licha ya kuwa anatumikia adhabu ya kutoruhusiwa kuingia uwanjani kwa kipindi cha miezi sita, adhabu iliyotolewa Juni 8, 2026.
Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya NBC kati ya Azam FC na Simba SC uliomalizika kwa Simba kushinda 2-0, Azam FC imepewa onyo kali kwa kutofuata mtiririko wa matukio ya mchezo.
TPLB imesema wachezaji wa Azam waliingia uwanjani kwa ajili ya kupasha misuli joto saa 12:07 jioni badala ya saa 12:10 jioni kama ilivyokuwa imeelekezwa na Mratibu wa Mchezo.
Kwa upande mwingine, Afisa Ulinzi na Usalama wa Azam FC, Masoud Fupe, amepelekwa Kamati ya Maadili ya TFF kwa kosa la kuvuruga utaratibu wa kuingia uwanjani kwa benchi la ufundi na wachezaji.
Fupe anatuhumiwa kuwaingiza viongozi wa benchi la ufundi la Azam, akiwemo Kocha Mkuu Frolent Ibenge, Kocha Msaidizi Anicet Makiadi pamoja na mchezaji Himid Mao, kupitia mlango usio rasmi, licha ya makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha maandalizi ya mchezo kuhusu mlango uliopaswa kutumika.
Katika mchezo wa Kagera Sugar na Fountain Gate uliomalizika kwa sare ya 1-1, waamuzi Hassan Mhina na Soud Hussein wameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitatu kutokana na kuonyesha mapungufu ya kiuchezeshaji yaliyotokana na kushindwa kutafsiri vizuri sheria za mpira wa miguu katika mchezo huo.
CHAMPIONSHIP
Katika Ligi ya Championship ya NBC, Bigman FC imepewa onyo kali kwa kosa la kuwakilishwa na wajumbe watatu badala ya watano katika kikao cha kitaalamu cha maandalizi ya mchezo dhidi ya IAA FC.
Aidha, Songea United imetozwa faini ya Sh milioni 5 kwa kushindwa kuvaa jezi zenye nembo ya mdhamini mkuu wa Ligi ya Championship ya NBC, licha ya kukumbushwa kufanya hivyo.
Maamuzi hayo yametolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Septemba 19, 2026.


