
Jan Ravnik, dansa aliyewahi kuwa sehemu ya kikosi cha Taylor Swift kwenye ziara yake ya Eras Tour, amefichua furaha yake baada ya kufanikiwa kununua nyumba yake mwenyewe nchini Marekani.
Ravnik, mwenye umri wa miaka 31 na raia wa Slovenia, alishirikisha picha za nyumba hiyo kwenye mitandao ya kijamii huku akieleza safari yake ya miaka kadhaa tangu alipohamia Marekani akiwa na kiasi cha dola 1,200 sawa na TSh 3,174,000 pekee kwenye akaunti yake.

Katika ujumbe wake, Ravnik alisema hatua hiyo ni moja ya mafanikio makubwa kwake baada ya kupitia changamoto mbalimbali na kufanya kazi kwa bidii ili kujenga maisha yake nchini humo.
“Leo ninaweza kusema kwa fahari… mimi ni mwenye nyumba,” aliandika Ravnik katika ujumbe wake, akifuatisha na emoji za furaha na upendo.
Alieleza kuwa alipohamia Marekani miaka isiyozidi 10 iliyopita, alikuwa na fedha kidogo na lengo lake kubwa lilikuwa kufanya kazi kwa bidii na kuthibitisha kuwa alikuwa na uwezo wa kuendelea kuishi na kufanya kazi katika tasnia hiyo.

Ravnik pia alieleza kuwa safari yake haikuwa rahisi, akitaja kuwa imeambatana na dhabihu nyingi, changamoto na vipindi vya kupanda na kushuka kabla ya kufikia hatua hiyo.
Picha alizoshirikisha zinaonyesha akiwa ndani ya nyumba hiyo mpya, huku moja ikimwonyesha akiwa amekaa juu ya sehemu ya fireplace akiwa na tabasamu kubwa usoni. Picha nyingine inaonyesha sehemu ya ndani ya nyumba yenye njia za ukutani zenye umbo la duara na sakafu iliyowekwa vigae.
Katika picha nyingine, Ravnik alionekana akiwa ameshikilia funguo za nyumba yake huku macho yake yakionekana kuwa na machozi ya furaha.

Safari yake na Taylor Swift
Mbali na mafanikio hayo, Jan Ravnik amejulikana zaidi kwa mashabiki wa muziki kutokana na kuwa mmoja wa dansa waliokuwa sehemu ya Eras Tour ya Taylor Swift.
Ravnik alijiunga na ziara hiyo mwaka 2023 na kuendelea kuwa sehemu yake hadi mwaka 2024. Pia ameonekana katika baadhi ya video za muziki za Swift, zikiwemo “The Fate of Ophelia,” “I Can Do It with a Broken Heart” na “Karma.”
Kabla ya mafanikio hayo, Ravnik aliwahi kueleza furaha yake baada ya kupata nafasi ya kuwa sehemu ya Eras Tour, akisema hakuwahi kufikiria kuwa kijana kutoka mji mdogo nchini Slovenia angeweza kufika mbali kiasi hicho.
Sasa, miaka kadhaa baada ya kuhamia Marekani, Ravnik ameongeza hatua nyingine muhimu katika maisha yake kwa kuwa mmiliki wa nyumba, jambo alilolielezea kama matokeo ya safari ndefu iliyojaa kazi, kujituma na changamoto.